Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeelekeza kuwa katika mchakato wa uchujaji na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, mgombea aliyeshinda kura za maoni apewe kipaumbele cha kuteuliwa au kupendekezwa na vikao husika ili mchakato uendelee.
Kwa mujibu wa barua iliyonaswa na Jambo TV ambayo inaonesha kuwa ya tarehe 9 Agosti 2025 ikiwa imeandikwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, imeelezwa kuwa iwapo vikao vitaamua kutomteua mgombea aliyeongoza kura za maoni, ni lazima viwasilishe ushahidi usio na shaka wa kukiuka maadili mbele ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Aidha imeelezwa kuwa mwongozo huo unazingatia Kanuni ya Uteuzi katika Vyombo vya Dola, Toleo la Machi 2025 Fungu la Kwanza (5) na Fungu la Tatu (9)(1)(a), ukiwataka watendaji wa chama kuhakikisha vikao vinatenda haki ili kuepusha migawanyiko na malalamiko ndani ya CCM.
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa utekelezaji wa mwongozo huo ni muhimu kwa “mustakabali mwema, maendeleo na uhai wa chama,” akiwataka makatibu wa mikoa na watendaji wote kuzingatia Katiba, Kanuni na miongozo ya CCM wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.