Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema chama chake kitafurahia kama vyama vingine vya siasa vitachangia kufanikisha kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa CCM inatumikia Watanzania wote bila ubaguzi.
Dkt. Nchimbi ameyasema hayo wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari Jumatatu Agosti 11, 2025 katika ofisi ndogo ya CCM Makao Makuu, Lumumba, mkoani Dar es Salaam
“Tutafarijika sana vyama vyote vikichangia, kwa sababu haihitaji ushahidi wa kipolisi kujua CCM inatumikia Watanzania na vyama vingine vyote. Si kosa kwa vyama vingine kusaidia chama hiki kinachotumikia watu wote kwa upendo,” amesema Dkt. Nchimbi.
Dkt. Nchimbi amebainisha kuwa harambee ya kitaifa ya kuchangia kampeni itazinduliwa rasmi kesho saa 11 jioni katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Harambee hiyo inalenga kukusanya Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya maandalizi ya kampeni, ikiwemo gharama za magari, mabango, mafuta, fulana na kanga.
“Tunachokusudia kupata kwa kiwango cha kawaida ni Bilioni 100, wanasiasa kokote walipo wajue hiyo ndiyo target tunayokusudia,” amesema.
Dkt. Nchimbi amesema kuwa harambee hii imekuja kufuatia hamasa kubwa ya wanachama wa CCM kutaka kuchangia kampeni baada ya chama hicho kutangaza kuwa kina wanachama zaidi ya milioni 13 waliothibitishwa kidijiti.