Latest Posts

GEITA MANISPAA YAPANDISHA MAKUSANYO, YAPITISHA BAJETI YA BILIONI 78.8

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, mkoani Geita, limepokea, kujadili na kupitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya shilingi bilioni 78.8.

Katika rasimu hiyo, makusanyo ya mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 23, ikiwa ni ongezeko la asilimia nane ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita ambapo zilikusanywa shilingi bilioni 22.

Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa rasimu hiyo ya bajeti, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Leonard Bugomola, amewataka madiwani pamoja na wataalamu wa halmashauri kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo katika ukusanyaji wa mapato. Amesisitiza umuhimu wa kusimamia kwa karibu vyanzo vyote vya mapato, hususan vile ambavyo awali havikuwa vikichangia ipasavyo, ili viweze kuongeza tija kupitia usimamizi mzuri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Miyenze, amesema bajeti hiyo itaelekezwa katika kuboresha huduma za jamii, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, kuimarisha sekta ya elimu pamoja na kuboresha mazingira ya shule kongwe ndani ya manispaa hiyo.

Nao baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo wamesema bajeti iliyopitishwa inatarajiwa kuwa suluhisho kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, ikiwemo miundombinu na huduma za kijamii, hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika manispaa ya Geita.

Kwa kupitishwa kwa rasimu hiyo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Halmashauri ya Manispaa ya Geita inatarajia kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuharakisha maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi, huku ushirikiano kati ya madiwani, wataalamu na wananchi ukitajwa kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa bajeti hiyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!