Wazazi na walezi mkoani Geita wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwaandikisha watoto wao shule mapema, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya muhula mpya wa masomo wa mwaka 2026, huku wakiondolewa tabia ya kusubiri kulazimishwa au kufuatiliwa na mamlaka husika.
Hadi sasa, kati ya Halmashauri tano zilizopo mkoani humo, Halmashauri ya Nyang’hwale inaongoza kwa zoezi la uandikishaji ambapo wanafunzi 5,368 sawa na asilimia 73 wameandikishwa kwa elimu ya awali, huku wanafunzi 6,539 sawa na asilimia 87 wakiwa wameandikishwa kujiunga na darasa la kwanza.
Akizungumza kuhusu hatua ya uandikishaji, Afisa Elimu Mkoa wa Geita, Mwalimu Antony Mtweve, amesema ni muhimu kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawaandikisha watoto wao kwa wakati uliopangwa na Wizara ya Elimu ili kuepuka changamoto zisizo za lazima.
Aidha, Mwalimu Mtweve ameongeza kuwa watoto wote wana haki na fursa ya kupata elimu bora, wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum, na kusisitiza kuwa ni vyema wazazi wakaachana na fikra potofu zisizo na tija kwa maendeleo ya jamii.
Kwa ujumla, Ofisi ya Elimu Mkoa wa Geita inaendelea kuhimiza ushirikiano wa wazazi na walezi katika kuhakikisha watoto wote wanaandikishwa shule kwa wakati, ili kutimiza lengo la Serikali la kutoa elimu jumuishi na bora kwa watoto wote bila ubaguzi, ikiwa ni maandalizi ya muhula mpya wa masomo wa mwaka 2026.