Latest Posts

HAYA NDIYO ATAKAYOLIPA MWIJAKU KWA KUSHITAKIWA NA KIPANYA MAHAKAMANI, ZIMO BILIONI 5.5 NA RIBA JUU

Mchoraji wa katuni maarufu nchini Tanzania na kimataifa ambaye pia ni mbunifu na mtangazaji wa vipindi vya redio na televisheni Ally Masoud Nyomwa (Masoud Kipanya) amefungua mashitaka Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Ndogo ya Dar es Salaam) dhidi ya Burton Mwemba (Mwijaku) anayemtuhumu kumkashifu, kumshushia hadhi na heshima yake kupitia maandishi kwenye mitandao ya kijamii.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Wakili wa Kipanya Alloyce Komba kutoka Haki Kwanza Advocates, Mahakama Kuu imepokea na kuisajili kesi hiyo (Namba 18911 ya 2024) tarehe 05 Agosti 2024, na Jaji David Ngunyale ndiye atakayeisikiliza kuanzia tarehe 03 Septemba 2024.

“Mdaiwa au mlalamikiwa (Bw. Burton Mwijaku) ameshapelekewa wito wa kuitwa mahakamani (summons to file written statement of defence) na kutakiwa kuwasilisha maelezo ya utetezi ndani ya siku 21 tangu alipopokea huo wito au samansi”, imeeleza taarifa hiyo.

Kipanya amemshitaki Mwijaku kwa kumkashifu kwa maandishi mnamo tarehe 04 Juni 2024 kupitia ukurasa wake wa Facebook wenye utambulisho namba 108657908847651 na kwenye akaunti yake ya Instagram aliyoandika maneno ya uongo, yenye nia ovu na kumfedhehesha yakiwemo kwamba yeye Kipanya anafanya biashara haramu inayoharibu maisha ya vijana wengi nchini.

Aidha, Kipanya ameeleza katika hati yake ya mashitaka kwamba Mwijaku aliandika kwenye akaunti za mitandao tajwa kwamba yeye Kipanya huwazodoa na kuwadhalilisha viongozi wa nchi na serikali hususani Marais kwa kuhongwa.

Kutokana na hayo yote, Kipanya ameiomba mahakama pamoja na mambo mengine imuamuru Mwijaku kumlipa fidia ya Shilingi milioni 500 ya madhara halisia (specific damages) atakayothibitisha kwa ushahidi mahakamani na fidia ya madhara ya jumla (general damages) yatakayopimwa na kuridhiwa na mahakama kwa mamlaka yake ya Shilingi bilioni tano.

KP ameomba pia malipo ya kiadhabu kwa mdaiwa yaani punitive damages na kwamba malipo ya fidia ya madhara halisia yaambatane na riba ya asilimia thelathini na moja (31%) tangu kashfa ilipotolewa yaani tarehe 04 Juni 2024 hadi utekelezaji wa hukumu utakapokamilika.

Aidha, Kipanya ameiomba mahakama katika hukumu yake itamke kwamba maneno yaliyoandikwa na kusambazwa na Mwijaku yalikuwa ni ya uongo, yenye nia ovu na ya kuharibu hadhi na heshima yake., na Mahimuamuru Bw. Mwijaku kuomba radhi bila masharti yoyote na kuondoa mitandaoni maneno ya kashfa yaliyoandikwa na kusambazwa.

Kipanya amesema maneno hayo ya uongo na yenye nia ovu yaliyochapishwa mitandaoni na kusomwa na watu wengi ndani ya jamii ya Tanzania na duniani kote, yametafsiri kwamba Masoud siyo mtu mwenye tabia nzuri wa kupewa heshima yoyote kwani hafai, anajihusisha na biashara haramu kama dawa za kulevya au nyara za serikali au magendo, hivyo kipato chake kinatokana na biashara hiyo haramu na sio uchoraji katuni, utangazaji, ubunifu, ubalozi wa masuala ya jamii, ukurugenzi wa bodi za taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa.

“Burton Mwijaku kwa tafsiri ya watu wa kawaida ndani ya jamii kwamba yeye KP (Kipanya) anaonekana ni mla rushwa, jambazi, tapeli, laghai, asiyeaminika, chanzo cha vijana walioharibiwa maisha yao, na kwamba hapaswi kuhusishwa katika masuala yoyote ya kijamii ikiwemo kupewa fursa na kufanya kazi na taasisi za serikali ambazo amekuwa akijihusisha nazo hasa katika elimu na malezi ya vijana mashuleni na mitaani”, imeeleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa kutokana na maandishi ya ‘kashfa ya maneno ya uongo’ ya Burton Mwijaku aliyenukuliwa pia kukiri kufanya hivyo mbele ya vyombo vya habari mnamo tarehe 13 Juni 2024 alipoomba radhi bila kuchukua hatua ya dhati ya kumsafisha kimaandishi Masoud Kipanya, imemuathiri kiajira, kibiashara, kimahusiano ndani ya jamii ya Tanzania kuanzia kwenye familia yake, kisaikolojia na kumshushia hadhi na heshima aliyoijenga kwa “jasho na damu” kwa zaidi ya miaka thelathini na tano (35).

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!