Mjadala mkali umeibuka leo Oktoba 12, 2026 kati ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, kuhusu hali ya miundombinu ya barabara, kasi ya ujenzi, na uendeshaji wa uchumi wa nchi.
Mjadala huo umeanza baada ya Heche kuchapisha kipande cha video kwenye ukurasa wake wa Instagram kikionesha hali ya barabara inayounganisha Mbalizi, Iwiji, na Umalila mkoani Mbeya. Katika chapisho hilo, Heche alimuambatanisha (kum-tag) Msemaji Mkuu wa Serikali na kuhoji namna serikali inavyoweza kujenga uchumi shindani kupitia miundombinu inayokabiliwa na changamoto.
“Hii ni Barabara ya kutoka Mbalizi-Iwiji- Umalila…hii ni Barabara muhimu inaleta chakula mnachokula kutoka Mbeya vijijini ili mpate nguvu…. Uchumi gani unaweza kujenga kwa kutumia barabara za hovyo kama hizi? Gharama ya kuzalisha na kusafirisha mazao kufika sokoni inakua mara mbili zaidi…Hamna uwezo wa kutatua changamoto ndogo kama hizi za barabara, maji na shule!!! Njoo ujibu unavyojisikia kuwa na Barabara kama hii kwenye nchi yetu miaka 65 baada ya Uhuru?”, amehoji Heche huku akiendelea kuikosoa serikali kwa kudai kuwa imeshindwa kutatua kero za msingi za wananchi na kuihusisha na uzembe pamoja na ubadhirifu wa rasilimali.
Akijibu mapigo kwenye sehemu ya maoni chini ya chapisho hilo, Msigwa ameeleza kuwa serikali inatambua changamoto hizo na inafanya kazi kwa awamu kulingana na uwezo wa kiuchumi na ukusanyaji wa kodi.
“Ni sahihi kwamba nchi yetu haijafikia uwezo wa kujenga barabara zote kwa kiwango cha lami kwa wakati mmoja. Kazi ya ujenzi wa barabara inaendelea na hivi sasa kuna kilometa 2,550 za lami wakandarasi wapo site ujenzi unaendelea. Tunakwenda kwa awamu, hata hii itafikiwa. Nchi wakati inapata uhuru mwaka 1961 ilikuwa na kilometa 1,300 za lami leo kuna zaidi ya kilometa 12,000 za lami na kilometa zaidi ya 25,000 za changarawe ambazo zinapitika vizuri na zipo katika hatua mbalimbali za kuwekewa lami.”, ameeleza Msigwa.
Msigwa ameongeza kuwa mbali na barabara, serikali inatekeleza miradi mingine mikubwa ikiwemo ujenzi wa viwanja vya ndege mikoani, mradi wa reli ya kisasa (SGR), uzalishaji wa umeme, na miundombinu ya afya na elimu. Ametamatisha kwa kumshauri Heche kujenga hoja kwa staha na kuitaka jamii ikumbuke kuwa kasi ya maendeleo inategemea uzalishaji na ulipaji wa kodi wa Watanzania wenyewe.
Hata hivyo, takriban saa tatu baadaye, Heche alichapisha video nyingine ikionesha hali ya barabara kuu ikiwemo barabara ya kutoka Singida kwenda Babati na Arusha na kujibu hoja hizo za Msigwa. Heche amepinga takwimu za kilometa 12,000 za lami zilizotajwa na Msigwa, akidai kuwa barabara nyingi kuu zinakabiliwa na changamoto ya viraka na mashimo.
“Msigwa, ninatumai hizo Barabara za lami km 12,000 ulizotaja sio hizi tunazozijua. Yaani kama unahesababu haya mashimo ya viraka kutoka Dar- Mwanza – Mara, Dar- Tunduma, Dar – Arusha, Dar – Mtwara au Dodoma -Mtera to Iringa au hiyo ya kutoka Singida to Babati kama ndio lami za aina hiyo basi utakuwa hauko sawa kabisa…hizo hazina viwango vya kuitwa barabara za lami. Hizo ni barabara za changarawe zilizojazwa viraka vya lami.” Amedai Heche.
Aidha, Heche ameeleza kuwa ukuaji wa idadi ya watu na magari unahitaji miundombinu yenye viwango vya juu zaidi kama barabara za njia mbili-mbili (highways/bypasses). Pia amegusia historia ya ujenzi wa reli tangu enzi za wakoloni na kuhoji ongezeko la deni la taifa linalofikia zaidi ya trilioni 110, akisisitiza kuwa rasilimali nyingi kama madini, misitu, na ardhi zinapaswa kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.