Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martin Rueben Shigela, amewataka Wakuu wa Wilaya mkoani humo kutumia muda wao mwingi kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zinazowakabili, ikiwemo migogoro mbalimbali iliyopo ndani ya wilaya zao.
Shigela ameyasema hayo katika ghafla ya kuwaapisha Wakuu wa Wilaya wapya pamoja na Makatibu Tawala wapya waliopangiwa majukumu katika Mkoa wa Manyara, huku akiwataka viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Wakuu wa Wilaya kuendelea kusimamia kwa karibu suala la usalama katika maeneo yao, ikiwemo kuchukua hatua dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayoweza kuhatarisha maisha ya wananchi.
Viongozi hao pia wametakiwa kuimarisha maandalizi na utekelezaji wa hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata ulinzi na msaada wakati wa changamoto zinazoweza kujitokeza.
