Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu kusimamia malezi na maadili ya vijana pamoja na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kutumia mafundisho ya dini kuelimisha jamii na kukemea vitendo hivyo.
Wito huo umetolewa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia ya Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA), Wilaya ya Arumeru, inayolenga kuhamasisha jamii kushirikiana kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika wilaya hiyo.

Katika kuimarisha ushirikiano huo, Lugangira amefanya mazungumzo na viongozi wa BAKWATA Wilaya ya Arumeru, wakiwemo Sheikh wa Wilaya, masheikh, maimamu na makatibu kutoka kata mbalimbali wanaowakilisha misikiti 115, ambao wamekubali kuunga mkono kampeni hiyo.
Amesisitiza kuwa vitendo vya ubakaji na ulawiti dhidi ya watoto ni makosa ya jinai ambayo hayapaswi kufichwa au kumalizwa kifamilia kwa fedha, zawadi au makubaliano yoyote, bali vinapaswa kuripotiwa katika vyombo vya sheria.

Aidha, amewahimiza viongozi hao kushiriki katika Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia itakayoanza Novemba 25 hadi Desemba 10, kwa kutoa elimu, kusimamia malezi na kuhamasisha jamii kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.