Chama cha ACT Wazalendo kimetoa taarifa kali ya kulaani kile kinachodaiwa kuwa ni uvamizi na kushikiliwa kwa muda kwa Kiongozi wake wa Chama Mstaafu, Zitto Zuberi Kabwe, na maofisa wa Jeshi la Polisi usiku wa tarehe 14 Julai 2025, akiwa katika hoteli mkoani Lindi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Ester Thomas, tukio hilo lilitokea majira ya saa sita usiku, ambapo polisi kutoka wilaya na mkoa wa Lindi waliwasili katika hoteli aliyofikia Zitto na baadaye kumpeleka katika kituo cha polisi kwa mahojiano ya zaidi ya nusu saa, pasipo kufahamisha mara moja kosa lake.
“Hatimaye, baada ya majibizano ya muda mrefu, polisi, majira ya saa saba na dakika nane usiku, walieleza na kubainisha kwamba wanamshikilia Kiongozi wa Chama Mstaafu kwa kosa la kutoa kauli za vitisho, kwa mujibu wa kifungu cha 89(2) cha sheria ya makosa ya jinai. Polisi hao walieleza kwamba kauli hizo za vitisho zilitokana na hotuba ya Ndugu Zitto Kabwe aliyoitoa siku ya tarehe 10/07/2025, akiwa kwenye mkutano wa hadhara Tunduru Kaskazini”, imeeleza taarifa hiyo.
Zitto Kabwe ameeleza kuwa atatoa maelezo yote mahakamani na alikataa kueleza zaidi kwa polisi, akisisitiza kuwa hiyo ni haki yake ya kisheria. Aliachwa huru majira ya saa nane usiku bila masharti yoyote.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni, Zitto alitoa onyo kali kwa maafisa wa polisi na watendaji wengine wa serikali wanaoshiriki katika kile alichokiita uingizaji wa kura bandia kwenye uchaguzi, akisema chama hicho hakitasita kuchukua hatua hata kama mhusika ni askari wa vyombo vya ulinzi na usalama, onyo ambalo baadhi ya wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala ya siasa wamelieleza kuwa ndiyo huenda imesababisha Zitto kuhojiwa Polisi.
Akihutubia siku ya Alhamisi Julai 10, 2025 katika Jimbo la Tunduru Kaskazini, wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Zitto alieleza kuwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, ACT Wazalendo ilimkamata afisa wa polisi akiwa amepakia kura bandia kwa lengo la kuzisambaza kwenye kituo cha kupigia kura, akisisitiza kuwa chama hicho hakitavumilia tena majaribio yoyote ya kuvuruga uchaguzi kwa ‘mbinu chafu’ kama hizo.
“Ninataka nitangaze rasmi hapa, na maafisa wa polisi watusikie: hatutajali magwanda yao, hatutajali nyota zao, hatutajali mitutu yao. Polisi atakayebeba kura bandia ni halali yetu,” aliongea Zitto kwa msisitizo.
ACT imelieleza tukio la karibuni la Zitto kuhojiwa kama sehemu ya “mwenendo wa kihuni” na kielelezo cha “kuendelea kuporomoka kwa misingi ya utawala wa sheria nchini.”
“Tunalaani kwa vikali vitendo vilivyofanywa na maafisa wa polisi usiku wa kuamkia tarehe 14/07/2025, na vinavyoendelea kutokea nchini kote. Tunawakumbusha polisi kwamba wanajukumu la kujiendesha kwa weledi na haki; na kushindwa kufanya hivyo ni kulinajisi jeshi na kulifanya jeshi la polisi kuwa jeshi la kihuni, linaloendeshwa kihuni na wahuni”, amesema Ester Thomas katika taarifa hiyo.
Chama hicho kimetoa wito kwa wananchi kuendelea kuilinda Tanzania dhidi ya “uhuni na uporaji wa haki,” na kusisitiza kuwa Zitto Kabwe yuko salama na ataendelea na ziara ya “Operesheni Majimaji” ya kuhamasisha wananchi kulinda kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.