Na; mwandishi wetu
Jumanne ya Desemba 03.2024 Dkt. Faustine Ndugulile aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kigamboni, Dar es Salaam kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika tumempumzisha katika makazi yake ya milele katika makaburi ya Mwongozo, Kigamboni, hiyo ikiwa ni baada ya siku saba (7) za tafakuri za kitabu chake cha miaka 55 zilizompendeza Mungu aishi hapa Duniani
Tangu kutangazwa kwa kifo chake Novemba 27 mwaka huu, kumekuwa na hisia mseto kuhusu maisha ya marehemu Dkt. Faustine Ndugulile na kwa kiasi kikubwa kila mmoja aliyemfahamu na kumsikia alijaribu kumzungumzia vile anavyomfahamu, ni ngumu kurejea kila mmoja alisema nini juu yake lakini kwa ujumla ninachokiweza kukisema hapa ni kwamba kila niliyemsikia akimzungumzia au kuandika chochote kuhusu yeye alieleza kumbukizi njema za kukumbukwa kwa kila mmoja wetu, Mungu amlaze mahapa pema, Amina
Hata hivyo leo siko hapa kuangaza au kusimulia kuhusu historia na kifo cha marehemu Dkt. Faustine Ndugulile la hasha, bali niko hapa kuangaza na kusimulia deni kubwa alilotuachia kama Taifa kuhusiana na maisha yake na kwa kiasi kikubwa nitaangaza kuhusu nafasi mbili kubwa ambazo hadi umauti unamkuta zilikuwa kichwani mwake, moja ni ya Ubunge wa jimbo la Kigamboni na ya pili ni ile ya Mkurugenzi mteule wa WHO Kanda ya Afrika
Maswali na mijadala iliyokuwepo hapa nchini na pengine hata nje ya nchi ikizingatiwa kuwa marehemu Dkt. Ndugulile alikuwa ‘wa kimataifa’ ni kwamba nani atakayepokea kijiti chake?, naomba nieleweke hapa sizungumzii kurithi bali kupokea
Kuhusu nafasi ya Ubunge wa jimbo la Kigamboni naamini hakuna mjadala mkubwa sana, kwa kuwa ninavyojuwa mimi na hasa kwa ninavyowafahamu wanasiasa watu walijiandaa mapema sana kupokea kijiti hicho, sio tu kwa sababu wengi walijuwa kuwa asingegombea katika uchaguzi mkuu wa mwakani (2025) bali pia ni kutokana na hulka ya wanasiasa ambao inaelezwa kuwa pindi uchaguzi mmoja unavyomalizika wale walioshinda na wale walioshindwa wote kwa pamoja huwa wanajiandaa na uchaguzi unaofuata kama bado wana dhamira ya kuendelea kushika kiti husika
Hapa inaelezwa kwamba wale wanaoshinda wamekuwa wakifanya shughuli zao huku wakipambana kuhakikisha uchaguzi ujao wanashinda tena, lakini wale walioshindwa huwa wanapambana pia kuhakikisha uchaguzi ujao hawashindwi tena, na hiyo si dhambi bali ndio hulka ya wanasiasa na vyama vyao Duniani kote
Kwa wakati huu ambao tumebakiza kipindi kisichozidi miezi sita (6) hadi saba (7) hadi kushuhudia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likivunjwa na Taifa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu, bila shaka wanasiasa kutoka chama tawala (CCM) na hata wale wa vyama vya upinzani tayari wameshaanza kupigana vikumbo huko Kigamboni kitambo sana, kama utaitishwa uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi au kama itasubiriwa mchakato wa jumla wa uchaguzi mkuu yote kwangu hayana shida, kila la kheri kwao
Huo sio sehemu ya mjadala wangu hapa pia, kwa kiasia kikubwa msingi wa makala hii ni kuhusiana na kofia ya pili aliyokuwa anaishikilia marehemu Dkt. Faustine Ndugulile nayo ni ile ya Mkurugenzi mteule wa WHO Kanda ya Afrika, ilikuwa imani yetu kwamba mwishoni mwa mwezi Februari au mwanzoni mwa mwezi Machi 2025 tumuone Mtanzania mwenzetu akianza majukumu yake, ikizingatiwa kuwa ni miezi michache tu tumetoka kushangilia ushindi wake
Bila shaka kilio kikubwa cha Taifa kiko kwenye eneo hilo, nimemsikiliza vizuri sana Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokwenda nyumbani kwa marehemu kule Kigamboni kuhani msiba, katika yale aliyoyaeleza alijaribu kugusia namna Taifa linavyotumia nguvu kubwa ya ushawishi, muda na kubwa raslimali fedha kuhakikisha Mtanzania mmoja anashika nafasi za kimataifa, na bila shaka kama nchi tulishangilia tukiamini kwamba ushindi wa marehemu Dkt. Ndugulile umetafsiri kuwa nguvu, muda na fedha tulizotumia kama Taifa ili kupigania nafasi hiyo havijaenda patupu
Waswali walisema, safari hupanga Mungu lakini Binadamu sisi huwa tunaamuliwa tu, ndivyo ilivyo kwetu tunapogusia kifo cha Dkt. Faustine Ndugulile, wakati sisi tukipanga yetu kumbe Mungu ameamua kuhusu kiumbe chake, hatuna la kusema zaidi ya kumshukuru yeye kwa zawadi ya maisha ya Faustine, ahsante Mungu
Swali lililoko sasa hapa nchini ni kwamba itakuwaje?, kama wewe ni miongoni mwa wanaojiuliza swali hili nikujuze kwamba kifo cha Dkt. Faustine Ndugulile hakina mfano wake katika historia ya WHO sio tu kwa Kanda ya Afrika bali Ulimwenguni kote
Kama hujanielewa, ninachomaanisha ni kwamba katika historia ya Shirika la Afya Duniani (WHO) haijawahi kutokea kwa Mkurugenzi mteule kufariki Dunia kabla haijaanza kuitumikia nafasi hiyo (kama ilivyokuwa kwa Dkt. Ndugulile), kwa hiyo hii ni mara ya kwanza na bila shaka hatua zozote zitakazochukuliwa katika kuziba nafasi hiyo huenda zikaweka alama na kielelezo cha kufuatwa sio tu kwa WHO Kanda ya Afrika bali kwa Kanda nyingine zote na pengine hata kwa WHO makao makuu
Sasa kwenye mazingira kama haya, wadau wa masuala ya afya Ulimwengu kote wameanza kutofautiana kwenye mitazamano kuhusu njia sahihi ya kufuatwa; wapo wanaosema kwamba katika taratibu za mashirika mengine ya kimataifa ni kwamba nafasi zake huwa ni za ushindani hata iweje na katika hilo kwa kuwa aliyekuwa ameshinda (ambaye ni amefarikia kwa sasa) hakugombea nafasi hiyo peke yake bali alikuwa na washindani wake, na kwa sababu imekuwa hivyo basi ni busara kwamba yule aliyekuwa mshindani wake wa karibu yaani aliyeshika nafasi ya pili akabidhiwe kijiti hicho, na kama itakuwa hivyo basi kijiti hicho tutashuhudia kikienda kwa raia wa Niger Dkt. Boureima Hama Sambo, ingawa nafahamu pia jambo hilo linaweza kuwa gumu
Maana yangu hapa ni kwamba, katika kushinda kiti hicho Tanzania na washirika wake (yaani yale mataifa yote yaliyokuwa yanaiunga mkono Tanzania na mgombea wake) sidhani kama itakuwa rahisi kwao kukubaliana na maamuzi hayo ya kuteuliwa kwa Dkt. Boureima kuongoza WHO Kanda ya Afrika, na hoja yao ya msingi itajikita kwenye eneo moja tu kuwa mgombea huyo walimkataa kwenye sanduku la kura hivyo hatoshi kukalia kiti hicho
Hatua ya pili, ambayo kimsingi ndio inayopigiwa chapuo na wengi ni kuona WHO ikiitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Mawaziri wa Afya na wale wa Mambo ya Nje wa Afrika ili kwa pamoja watafute mwafaka wa jambo hilo, na kwa kiasia hapo ni matarajio ya wengi kuona uchaguzi mpya ukiitishwa yaani mchakato uanze upya
Sasa hapa ndipo penye mzizi wa makala hii, hivi karibuni wakati wa hafla ya kuaga mwili wa Dkt. Faustine Ndugulile pale kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliweka wazi msimamo wa Tanzania kwenye jambo hilo kuwa licha ya kwamba Taifa limepoteza lakini litasimama imara kutafuta Mtanzania mwingine mwenye sifa akapelerushe bendera ya nchi kwenye kinyang’anyiro hicho, maana yake ni kwamba Tanzania itaendeleza mapambano ya kuhakikisha kiti hicho kinakaliwa na Mtanzania kuanzia mwakani,
Najuwa wako Watanzania wengi wabobezi, hususani walioko kwenye kada ya afya wenye sifa ya kupeperusha bendera ya nchi kwenye eneo hilo, hapa tunakusogezea mtazamo na uchambuzi wa Jambo TV kwa Watanzania tunaoona wanatosha kutuwakilisha kwenye kiti cha Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, kama ifuatavyo:-
(i) Dkt. Hamisi Kigwangalla;
Huyu naweza kusema ana sifa zinazokaribiana kabisa au kufanana na marehemu Dkt. Faustine Ndugulile, hadi sasa yeye ni Mbunge wa jimbo la Nzega vijijini (CCM), kama ilivyo kwa Dkt. Ndugulile naye aliingia Bungeni kwa mara ya kwanza 2010, huyu ni Dakrari wa binadamu kitaaluma, na jambo la kufurahisha ni kwamba yeye ndiye aliyemuachia kijiti Dkt. Ndugulile kwenye nafasi ya Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Kama ilivyokuwa kwa Dkt. Ndugulile kwamba kuna wakati mamlaka ya uteuzi ilimteua kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nafasi ambayo ni tofauti kabisa na taaluma yake, huyu pia kuna wakati mamlaka ya uteuzi ilimteua kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii nafasi ambayo ni kinyume kabisa na taaluma yake aliyobobea
Wakati wa kuaga mwili wa Dkt. Ndugulile pale Karimjee, Waziri wa Afya wa Congo Brazzaville Gilbert Mokoki aliwaeleza waombolezaji kuwa miongoni mwa sifa zilizopelekea wamchague Dkt. Ndugulile ni kuwa alikuwa ndiye mgombea kijana kuliko wengine wote, itakumbukwa kuwa Dkt. Ndugulile hadi anafariki alikuwa na umri wa miaka 55, sasa kama wapiga kura waliangalia kigezo hicho basi Dkt. Kigwangalla anafaa sana kwa kuwa Tanzania itampeleka mgombea kijana zaidi mwenye umri wa miaka 49
Jambo lingine kubwa la ziada kutoka kwake ni kwamba ni miongoni mwa vijana wanaopenda kusimamia kile wanachokiamini bila kujali jamii itapokeaje, anaamini kwenye mijadala ya hoja lakini pia mtetezi haswa wa jambo lolote lililoko upande wake
(ii) Prof. Mohamed Janabi;
Kwa sasa yeye ni Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), bila shaka huyu naweza kusema ni miongoni mwa wanataaluma wabobezi wa afya waliojizolea umaarufu mkubwa nchini na pengine hadi nje ya mipaka ya Tanzania, ni ngumu kuanza kuchambua safari yake ya kielimu na ubobezi wake kwenye sekta ya afya kutokana na ukweli kwamba ni CV kubwa na iliyosheheni kweli kweli
Ni mkakati wa WHO na Dunia kwa sasa kuona katika kipindi hiki ambacho magonja yasiyoambukiza yanatajwa kuwa hatari zaidi, basi wataalamu wa kada ya afya wanapaswa kuhakikisha wanajikita kutoa elimu na chanjo ili watu wasifikie hatua ya kuugua, kwenye eneo hilo nadhani endapo Prof. Janabi atakalia kiti hicho ataisaidia sana Afrika ambayo inatajwa kuwa hatarini zaidi kwenye eneo hilo, huyu pia amewahi kuwa Daktari binafsi wa Rais wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005
Lakini hapa kuna mambo mawili naona yanaweza kuwa magumu kwa Tanzania kama nchi kumruhusu akagombee nafasi hiyo, moja ni kwamba nadhani Tanzania inamuhitaji zaidi na haiko tayari kumuacha akatumike kwingine kwa sasa kutokana na kazi kubwa na nzuri anayoifanya hapa nchini,
Lakini jambo la pili, kama kile alichokieleza Waziri wa Afya wa Congo Brazzaville kuhusu kuwapa nafasi vijana ni msimamo wa wengi nadhani huo ni mtihani mkubwa kwa Tanzania endapo itamruhusu Prof. Janabi kuwa mgombea wake
(iii) Prof. Abel Makubi;
Huyu kwa sasa ni Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, ni mmoja kati ya wataalamu wabobezi wa masuala ya afya nchini akijikita kwenye masuala ya mifuma, ametumikia Hospitali za umma na binafsi kwa nyakati tofauti ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando iliyoko jijini Mwanza, na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Naye ni miongoni mwa wabobezi wenye CV nzito amewahi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali lakini kubwa kuliko yote amewahi kuwa pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, wakati Rais Samia anapambana kubadilisha mitazamo ya Watanzania kuhusu UVIKO-19 inaelezwa kuwa miongoni mwa wachora ramani na wasimamizi wa jambo hilo alikuwa Prof. Abel Makubi, kwa watu waliofanyanao kazi wanamtaja kuwa ni miongoni mwa watu wenye msimamo mkali na anayetaka kuona matokeo kwenye kila jambo analolifanya
(iv) Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya;
Siku chache zilizopita Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua mbobezi huyu wa masuala ya afya ya mifupa kuwa Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), anatajwa kuwa Mtanzania kwanza nchini kupata mafunzo ya kibingwa ya anaesthesiologist
Huyu pia amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada kwa takribani miaka minne (4) kuanzia 2019 hadi 2023, wakati Hayati Dkt. John Pombe Magufuli anamteua kuwa Balozi kulikuwa na malalamiko na minong’ono mingi miongoni mwa wadau wa kada ya afya kwani wengi wao walidai kuwa hakustahili kuteuliwa nafasi nje ya taaluma yake aliyobobea kwani kufanya hivyo ni kama nchi inajifunga kutumia kipawa alichonacho kwenye ubobezi wake
Hata hivyo, katikati ya mjadala huo wapo wanaoamini kuwa uteuzi wake wa hivi karibuni unaweza kuwa na taswira mbili kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, moja ni kuendelea kumuongezea CV zaidi ikizingatiwa kuwa amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya huko nyuma lakini jambo la pili ni kwamba kitendo cha kuteuliwa kuwa Mkurugenzi mtendaji wa MOI ni dhahiri kuwa hayuko kwenye mipango ya wapeperusha bendera ya Tanzania WHO Kanda ya Afrika
(v) Dkt. Ntuli Kapologwe;
Kwa sasa huyu ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI)
Ukiacha wengine wote niliowataja hapo awali ambao kimsingi wote wamehudumu na wanaendelea kuhudumu kwenye sekta ya afya na ni wabobezi, lakini huyu ndio mtu pekee kati ya hao niliowataja ambaye ameanzia ngazi ya chini kabisa hadi kupata kufikia kuwa Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya
Amekuwa Daktari kwenye Vituo vya Afya kadhaa, kabla ya kuhamishiwa kwenye Hospitali, kisha baadaye akawa Mganga Mkuu wa wilaya (DMO), Mganga Mkuu wa mkoa (RMO) nk, huyu pia alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa mstari wa mbele kumpigia kampeni marehemu Dkt. Faustine Ndugulile
Kwa ujumla, Tanzania inayo raslimali watu wengi wanaoweza kupokea kijiti cha marehemu Dkt. Faustine Ndugulile na pengine wakapeperusha vyema bendera ya Tanzania katika uchaguzi wa kumpata mrithi wa Dkt. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika anayemaliza muda wake, Mungu Ibariki Tanzania.