Vijana mkoani Mtwara wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii vizuri ili iweze kuleta maendeleo na kuwanufaisha.
Akizungumza Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mtwara Mobutu Malima kwenye Fainali ya Mtenga Jimbo Cup Season 2 amewataka vijana kuacha kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo ambayo sio ya msingi na badala yake watumie katika michezo.
“Tutumie mitandao ya kijamii katika michezo,isifike mahala tukakosa kazi ya kufanya tukashindwa kutekeleza majukumu yetu tukaanza kutukana,kudhalilishana,kuzuliana fitina na uongo kwenye mitandao.”Amesema Mobutu
Aidha amewasisitiza vijana hao kutumia mitandao kwa kuhabarishana habari njema ambazo hazitokuwa sababu ya kufitinisha jamii,viongozi na wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini Hassan Mtenga amesema lengo la kuanzisha ligi hiyo ni kuanzisha timu ya Mtwara ambayo itakwenda kucheza kuanzia ligi daraja la kwanza hadi ligi kuu.
Amesema ligi hiyo imeendeashwa kwa kipindi cha miezi 3 ambapo wamefanikiwa kupata vijana zaidi ya 7 kutoka kwenye ligi hiyo ambapo lengo la wabunge wa Mtwara ni kupata timu itakayoitwa Mtwara Rangers.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mtwara mjini Salumu Naida amewataka wananchi kuendelea kushirikiana hata kwenye majukumu mengine na kwenye kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ambao utaanza rasmi Novemba 11hadi 20,2024.
Nao baadhi ya washiriki ligi hiyo wamempongeza Mbunge huyo kwa kuanzisha ligi ambayo inawakutanisha vijana kutoka kata zote zilizopo kwenye jimbo hilo na kupata fursa ya kufahamiana.