Kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za ujenzi kilichopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani cha Huaxin Metal Products kimedaiwa kuzalisha na kuuza bidhaa ‘feki’ ambazo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo bidhaa hizo zinapaswa kuharibiwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika, bidhaa hizo zilikamatwa na polisi waliokuwa katika operesheni mwanzoni mwa mwezi Desemba 2024 wakati zikishushwa kutoka kwenye gari aina ya Scania lenye namba T299 DCV njiani.
Bidhaa hizo ni vifaa vya ujenzi (plates 40 na square pipes zaidi ya elfu nne) ambazo kwanza imeelezwa kuwa hazikuwa na risiti lakini pia ikagundulika kuwa na walakini zaidi mara baada ya Wakala wa Vipimo (WMA) mkoa wa Pwani kupewa taarifa juu ya bidhaa hizo.
Chanzo chetu kinaeleza kuwa WMA Pwani iligundua kuwa vipimo vya square pipes havikushabihiana na viwango hitajika na pia hazikuwa na lebo, hivyo ukafanyika utaratibu wa kwenda kiwandani kulikokutwa mzigo mkubwa ulioelezwa kuwa na vipimo sawia na kama vya awali. Wamiliki wa kiwanda hicho walipewa amri ya kusimamisha uzalishaji na kuripoti ofisi za WMA, hata hivyo iliwachukua muda uongozi wa kiwanda hicho kuripoti ofisi za WMA Pwani ndani ya siku saba.
Kulingana na fomu ya ukaguzi wa Vipimo ya tarehe 5 Desemba 2024 ambayo JAMBO TV tuliiona kuhusu bidhaa hizo na ikiwa na sahihi ya Afisa Mkaguzi na Sahihi ya Mmiliki wa Kiwanda ilinukuliwa kama ifuatavyo.
“Imekaguliwa na kuonekana Square pipes zinazalishwa na kuuzwa bila kuwa na ‘labelling’ kinyume cha Sheria ya Vipimo Sura ya 340 Mapitio ya Mwaka 2002, pia ziko na upana 0.9mm, Length 4. 17m”
Inaelezwa kuwa baada ya wamiliki wa kiwanda hicho kuonekana kutotilia maanani wito wa kufika ofisini, hatimaye walifika ili kufuata utaratibu wa kisheria wa WMA ambao unahusisha kuteketeza mali ambazo hazipo sahihi.
Kulingana na chanzo chetu, ili kukamilisha hatua ya uharibifu wa bidhaa ‘feki’ ni lazima mmiliki aweke sahihi yake kwenye fomu ya faini (penati ya serikali) hata hivyo kwa upande wa uongozi wa Huaxin hali ilikuwa tofauti. Uongozi wake ulikataa kusaini fomu hiyo ukieleza kuwa ungeweza kufanya hivyo tu mpaka pale mwanasheria wao atakapokuwepo. Baada ya kuwa na msimamo huo, WMA iliwapa siku tatu kukamilisha zoezi la kusaini lakini mpaka habari hii inachapishwa tarehe 31 Desemba 2024, uharibifu wa bidhaa hizo unaonekana kutofanikiwa.
Jambo TV tulimtafuta Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA Alban Kihulla kutaka kufahamu zaidi juu ya hatua zilizochukuliwa kutokana na kukamatwa kwa bidhaa hizo, akasisitiza kuwa jambo hilo linaweza kuelezwa zaidi na WMA mkoa wa Pwani kwakuwa ni sehemu ambayo tukio hilo lilitokea.
Jambo TV tukaona hiyo haitoshi, tukautafuta kwa njia ya simu uongozi wa kiwanda hicho kupata mtazamo wao lakini simu hiyo haikupatikana ikatulazimu kusafiri kigulu na njia kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanambaya, Mkuranga mkoani Pwani kilipo kiwanda hicho siku ya Jumamosi tarehe 28, Desemba 2024. Hata hivyo tukakuta shughuli katika kiwanda hicho zinaendelea kama kawaida, kisha tukapokelewa na Mkuu wa Ulinzi wa Kiwanda hicho ambaye alitueleza kuwa hakuna changamoto yoyote katika kiwandani na kama ingelikuwepo basi angelikuwa na taarifa.
Katika kutaka kufahamu kipi kinaendelea katika sakata hilo, Jambo TV ilimtafuta njia ya simu siku hiyohiyo ya Jumamosi, Meneja WMA mkoa wa Pwani, Hashim Athumani ambaye alitupa mwaliko wa kufika ofisini kwake wilayani Kibaha mkoani Pwani siku ya Jumatatu Desemba 30, 2024 ambako tulifika, hata hivyo tukaelezwa kuwa kulikuwa na ugeni maalumu siku hiyo, na tukaambiwa tuje siku inayofuata ambayo ni Jumanne ya tarehe 31 Desemba 2024.
Mapema asubuhi ya siku ya Jumanne, tukampigia kwa simu Meneja huyo bila mafanikio, tukamtumia ujumbe wa simu wa kawaida na kupitia mtandao wa WhatsApp lakini licha ya ujumbe huo kuonekana kufika na kupokelewa, haukujibiwa.
Sakata hili linaibua wasiwasi wa JAMBO TV kuhusu kusuasua kwa serikali katika kuchukua hatua za kisheria kwa kiwanda ambacho kimedhihirika bayana kuzalisha bidhaa zilizo chini ya kiwango.
Jambo TV inaendelea kufuatilia suala hili kwa ukaribu ili kuhakikisha maslahi ya wananchi yanazingatiwa kwa kulindwa dhidi ya bidhaa zisizo salama.