Msimu wa nne wa Korosho Marathon unatarajiwa kunufaisha vikundi vya wabanguaji wadogo wa korosho kwa kuwapatia mashine za umeme zitakazowarahisishia kazi ya ubanguaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Revelian Ngaiza amesema kuwa lengo la Korosho Marathon ni kuhamasisha ulaji wa korosho, kupanua soko hasa la ndani, pamoja na kuhamasisha ubanguaji. Kupitia marathon hiyo, watagawa mashine za umeme kwaajili ya kubangua korosho.

Ameongeza kuwa wakulima wengi wanatamani kubangua korosho lakini hukumbana na changamoto ya vifaa hivyo, watatoa mashine 50 za umeme kwa vikundi walivyokubaliana navyo, ili kurahisisha ubanguaji wa kilo 600 kwa siku ambapo katika msimu wa mwaka juzi waligawa mashine 20 kwa vikundi vya Mtwara na Lindi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya, amesema ujio wa Korosho Marathon utaleta fursa kubwa kwa wajasiriamali wa mkoa huo kutokana na ujio wa watu zaidi ya elfu tatu, jambo litakalosaidia kuongeza uchumi wa wananchi na kuchochea maendeleo ya wajasiriamali.
Aidha, amewahakikishia usalama wananchi wote wa Mtwara na wale kutoka nje ya mkoa katika tukio hilo kubwa, ili waweze kufika na kujionea fursa zilizopo na amewashukuru wadau wote 17 waliojitokeza kudhamini tukio hilo.

Kwa upande wa wadau wa korosho, ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele Humphrey Mlimbila wamesema wameona umuhimu wa kudhamini tukio hilo ili kutoa elimu kuhusu uongezaji thamani wa zao la korosho.