Kuelekea msimu wa nne wa Korosho Marathon, jamii ya Mtwara imeendelea kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazojitokeza kupitia tukio hilo, huku wajasiriamali na taasisi binafsi wakionekana kutumia vyema uwepo wa marathon hiyo kuongeza kipato na kukuza biashara zao.
Katika maandalizi ya mwaka huu, mandhari ya Korosho Marathon imeendelea kuvutia sio tu kwa mbio za michezo, bali kwa wingi wa huduma na shughuli mbalimbali zinazofanyika pembeni ya tukio hilo huku huduma za nyama za kuchoma za wanyamapori, maonyesho ya wanyama kama Pundamilia, Tausi, Simba na Nyati pamoja na michezo ya watoto, vimechangia kuongeza mwamko wa wananchi kushiriki na kutumia huduma za wafanyabiashara wa eneo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mkemi Agrix Company Limited, Salum Mkemi, anasema tukio hilo limekuwa chachu ya kukuza thamani ya korosho ndani ya nchi kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwahimiza kutegemea zaidi soko la ndani ambalo linaonekana kuwa na uthabiti kuliko soko la nje lenye mabadiliko ya mara kwa mara.

Kwa upande wa elimu ya kifedha na kilimo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Korosho Marathon, Revelian Ngaiza, amesema taasisi mbalimbali za kifedha zitakuwepo kutoa elimu ya huduma za fedha ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu mikopo na uwekezaji na kuongeza kuwa maandalizi yamepokelewa vizuri, na zaidi ya washiriki 1,500 wamejisajili tayari.
Ushiriki wa wananchi na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kumeifanya Korosho Marathon kuonekana zaidi kama jukwaa la maendeleo ya jamii tukio linalochangia kuongeza kipato, kuhamasisha utalii wa ndani, na kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu kilimo cha korosho.