Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaomba wakazi wa Ngerengere, Mkoa wa Morogoro, kuwachagua wagombea wa CCM katika nafasi zote tatu za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza leo, Ijumaa Agosti 29, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Ngerengere, Morogoro Vijijini, Dkt. Samia amewataka wananchi kuhakikisha kura zao zinaenda kwa CCM kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani ili chama hicho kiendelee kutekeleza mipango yake ya maendeleo.
Aidha, akitumia mfano wa michezo, amesema baadhi ya vyama vya upinzani vimekata tamaa mapema na kushindwa kuonesha nia ya ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samia amesema serikali yake imejipanga kushughulikia changamoto ya maji katika Mkoa wa Morogoro kwa kutekeleza miradi mipya na kulinda vyanzo vya maji.
Amesema serikali imetekeleza miradi 15 ya maji tangu mwaka 2020, hatua iliyoongeza upatikanaji wa huduma hiyo kutoka asilimia 51 hadi asilimia 57.
Hata hivyo, alikiri bado kuna changamoto kubwa katika maeneo kadhaa, ambayo ni muhimu kwa kilimo cha umwagiliaji. Rais Samia ameeleza kuwa tatizo hilo linachangiwa na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti na uchomaji wa mkaa kupita kiasi, hali inayosababisha vyanzo vya maji kukauka.
Ameongeza kuwa eneo la maji limepewa kipaumbele maalum katika mpango wa serikali yake kwa miaka mitano ijayo, likiwemo kuhakikisha miradi ya umwagiliaji inafanikiwa na huduma ya maji inawafikia wananchi wengi zaidi.