Katika juhudi za kuhamasisha uchumi mbadala na kupunguza utegemezi wa shughuli haramu kama uwindaji na uchomaji wa mkaa, utengenezaji wa batiki umetajwa kuwa mkombozi mpya kwa wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Grumeti na mapori ya akiba wilayani Serengeti, mkoani Mara.
Nelson Petro, Afisa Mradi wa Ustawishaji Biashara Vijijini kutoka Shirika la Grumeti Fund, amesema hayo wakati wa mafunzo ya utengenezaji wa batiki kwa wanafunzi yaliyofanyika katika kijiji cha Parknyigoti, moja kati ya vijiji 21 vinavyonufaika na mpango huo.

“Tunataka jamii inayozunguka eneo hili iwe endelevu kiuchumi, iwe na fursa mbadala za kipato na iwe mstari wa mbele katika kulinda mazingira. Batiki ni moja ya njia tulizoziona zinaweza kusaidia kutimiza hilo,” alisema Petro.

Kubadili Mwelekeo wa Maisha Vijijini
Petro alieleza kuwa kwa miaka mingi, baadhi ya wananchi waliokuwa wakitegemea uwindaji haramu na uchomaji wa mkaa kwa ajili ya kujipatia kipato sasa wanapewa mbinu na maarifa ya kutengeneza batiki kama njia ya kujikimu, huku wakihifadhi mazingira na kudumisha rasilimali za asili.
“Tunachofanya ni kuandaa vijana na wanawake wa vijiji hivi kuwa na ujuzi wa utengenezaji wa batiki, bidhaa ambayo ina soko la uhakika ndani na nje ya nchi, huku tukiwaepusha na shughuli za uharibifu wa mazingira,” aliongeza.
Kijiji cha Parknyigoti Chafaidika
Kijiji cha Parknyigoti kimeelezwa kuwa mfano bora wa mabadiliko haya, ambapo wanafunzi na wanajamii wameonyesha hamasa kubwa katika kujifunza na kuanza kutengeneza bidhaa hizo za batiki, ambazo zimeanza kuingia sokoni na kuongeza kipato cha kaya nyingi.

Lengo Kubwa: Uhifadhi na Ustawi wa Jamii
Grumeti Fund kupitia mradi huu inalenga kusaidia zaidi ya vijiji 20 vinavyopakana na hifadhi, kwa kuwajengea uwezo wa kutumia ujuzi wa batiki kama njia endelevu ya kujipatia kipato bila kuathiri mazingira.