Latest Posts

LAINI ZA SIMU ZAFIKIA MILIONI 106.9 NDANI YA SIKU 100 ZA UONGOZI WA RAIS SAMIA

‎Idadi ya laini za simu zilizosajiliwa nchini imeongezeka kutoka laini milioni 99.3 mwezi Oktoba 2025 hadi kufikia laini milioni 106.9 mwezi Januari 2026, sawa na ongezeko la asilimia 7.7 ndani ya siku 100 za uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‎Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 04 Februari, 2026, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesema ongezeko hilo limetokana na uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ikiwemo minara ya mawasiliano na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

‎Waziri Kairuki  amesema kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti nayo imeendelea kuongezeka, ambapo imepanda kutoka milioni 56.3 mwezi Oktoba 2025 hadi milioni 58.1 mwezi Januari 2026, sawa na ongezeko la asilimia 3.2.

‎Aidha, huduma za kifedha kupitia simu Waziri Kairuki amesema zimeendelea kushika kasi, ambapo watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea fedha kwa njia ya mtandao wa simu wameongezeka kutoka milioni 71.7 hadi milioni 76.5 katika kipindi hicho, sawa na ongezeko la asilimia 6.7.

‎Kwa upande wa gharama za mawasiliano, Waziri Kairuki amesema Serikali imeendelea kudhibiti gharama ili kuwezesha wananchi wengi kumudu huduma hizo, ambapo gharama za kupiga simu ndani ya nchi zimeendelea kuwa Shilingi 29 kwa dakika, huku wastani wa bei ya data bila kifurushi ukiendelea kubaki Shilingi 9.35 kwa kila MB 1.

‎Amesema kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za mawasiliano na Teknolojia ya Habari, hususan katika maeneo ambayo awali hayakuwa na huduma, kumeongeza upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kidijitali ikiwemo huduma za kifedha na afya, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

‎Katika kuhakikisha vijana wabunifu wanakuwa na chanzo cha uhakika cha fedha, Waziri Kairuki alisema Wizara imeanza maandalizi ya kuanzisha Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji wa Kampuni Changa za TEHAMA (ICT Startups Development Fund), ambao utawezesha upatikanaji wa mitaji kwa kampuni changa ambazo mara nyingi hukosa fursa ya kupata mikopo kutoka benki na taasisi za fedha.

‎Ameongeza kuwa mfuko huo utakapokamilika utasaidia vijana kuanzisha na kukuza biashara zao, kuboresha bidhaa na huduma wanazozitoa pamoja na kuwafikia masoko kwa haraka zaidi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga uchumi wa kidijitali

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!