Latest Posts

LAKE MANYARA MARATHON: FURSA YA KUINUA UTALII NA MICHEZO TANZANIA

Mratibu wa mashindano ya Lake Manyara Half Marathon, Bi. Maureen Morris Okinda, amewaalika wananchi na wapenda michezo kushiriki katika msimu wa pili wa mbio hizo, zitakazofanyika tarehe 30 Novemba 2024, katika eneo la Monduli, Mto wa Mbu.

Bi. Okinda amesema mashindano hayo yatakuwa na mbio za umbali wa kilomita 21, kilomita 10, na mbio za burudani za kilomita 5. Washiriki wote wanatakiwa kulipa ada ya ushiriki ya shilingi 35,000 za Kitanzania ili kuweza kushiriki katika mashindano hayo yanayoendelea kupata umaarufu zaidi nchini.

Akizungumzia kuhusu zawadi kwa washindi, Bi. Okinda alieleza kuwa washindi wa mbio za kilomita 21 kwa upande wa wanaume watapata zawadi kubwa ambapo mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi 600,000, huku nafasi nyingine za juu pia zikitarajiwa kutoa zawadi ya fedha taslimu. Kwa upande wa wanawake watakaoshiriki mbio za kilomita 10, zawadi ya mshindi wa kwanza ni shilingi 500,000, huku wengine pia wakitarajiwa kupata zawadi kwa nafasi mbalimbali.

Bi. Okinda ametoa wito kwa wadau mbalimbali, pamoja na washiriki wa michezo, kujitokeza kwa wingi ili kuunga mkono tukio hili ambalo lengo lake ni kuinua sekta ya utalii kupitia michezo, pamoja na kuchangia maendeleo ya jamii. Pia, alitaja mafanikio ya mashindano ya msimu wa kwanza mwaka 2023 kama ishara ya ukubwa na mafanikio yanayotarajiwa kwa msimu huu wa pili.

Mashindano haya yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wakimbiaji wa viwango mbalimbali, na pia yamechangia kuvutia watalii kwenye eneo la Lake Manyara, huku yakiwa chachu ya kukuza uchumi na afya ya jamii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!