Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasri Ally, amewataka maofisa ugani walioajiriwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kuwapa elimu wakulima wa korosho mkoani Pwani ili waweze kunufaika zaidi kiuchumi kupitia kilimo hicho.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa maofisa ugani yaliyofanyika mjini Mkuranga, Khadija alisema wakulima wengi wanatumia mbinu za kizamani zisizoleta tija. Alisisitiza maofisa ugani kuwafundisha wakulima mbinu bora za kilimo ili waweze kupata faida.
Wakulima wanapaswa kufundishwa jinsi ya kutunza mikorosho yao, ikiwemo upuliziaji sahihi wa dawa, muda unaofaa wa kupulizia, pamoja na umuhimu wa kupalilia mashamba yao. Haya yote yataongeza mavuno na faida katika kilimo cha korosho, alisema.
Khadija aliongeza kuwa iwapo mkulima atahamasishwa na kunufaika na kilimo, ataendelea kulima kwa bidii. Aidha, alisisitiza umuhimu wa programu mbalimbali za serikali zinazolenga kuwasaidia vijana kujiajiri kupitia fursa za kilimo.
Khadija alieleza majukumu muhimu ya maofisa ugani hao, ambayo ni kuhuisha kanzidata ya wakulima wa korosho, kusimamia usambazaji wa pembejeo kwa wakulima, kutoa elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu, kufufua mashamba pori ya korosho, kusimamia ubora na mfumo wa uuzaji wa korosho, kuwatembelea wakulima mashambani na kuwashauri mbinu bora za kilimo, na kukusanya takwimu za korosho zinazobaki majumbani kwa ajili ya kujumuishwa katika uzalishaji wa kitaifa.
Nendeni mkawasaidie wakulima kwa utaalamu stahiki. Zao la korosho ni zao la kiuchumi na kimkakati kwa taifa, hivyo lazima tuliendeshe kisayansi ili kila mtu anufaike, alisema Khadija.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Bodi ya Korosho CBT, Domina Mkangara, alisema mafunzo hayo yatakuwa na manufaa kwa wilaya sita za mkoa wa Pwani zinazozalisha korosho kwa wingi. Alisema mafunzo hayo yana lengo la kusogeza huduma za maofisa ugani karibu na wakulima, hasa kutokana na changamoto ya uhaba wa huduma hizo.
Mkangara alibainisha kuwa mafunzo hayo yameandaliwa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo ili kuongeza idadi ya wataalamu wa kilimo cha korosho kuanzia hatua za uzalishaji hadi uuzaji.
Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdalah Ulega, Msaidizi wake Shein Kilindo alisema mafunzo hayo yatasaidia vijana wanaojishughulisha na kilimo cha korosho wilayani humo.
Zao la korosho ni tegemeo kwa vijana wa Mkuranga, lakini wengi hulima kienyeji bila utaalamu, jambo linalosababisha wakose faida. Mafunzo haya yatakuwa msaada mkubwa kwao, alisema Kilindo.