Na Josea Sinkala, Mbeya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya Erica Yegella, amewataka watumishi katika Halmashauri hiyo kushirikiana katika kuwatumikia wananchi badala ya kusubiri kusukumwa kufanya kazi.
Mkurugenzi huyo mpya wa Halmashauri ya Mbeya, ameeleza hayo Januari 29, 2025 wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Amesema baada ya kuripoti katika Halmashauri ya Mbeya, tayari amefanya kikao na watumishi hasa idara ya mipango na kuwasisitiza kwenda kufanya kazi kwa weledi na uadilifu kwa maslahi mapana ya wananchi ambao ndio walipa kodi.
Amesema Serikali lazima iishi kwa vitendo dhana ya kazi iendelee kwa kuhakikisha watumishi wanatoka ofisini na kwenda kuwatumikia wananchi ikiwemo kumalizia miradi mbalimbali inayoendelea na kuendelea na utekelezaji miradi mbalimbali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya Mhe. Mwalingo Kisemba, amewashukuru waheshimiwa madiwani wa Halmashauri yake kwa kushirikiana na wataalam kwenye maeneo yao kuendelea kufanya kazi na usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.