Mkuu wa Mkoa wa Lindi Adam Malima amewataka viongozi, watendaji wa Serikali na wananchi wa Mkoa wa huo kukaa pamoja, kuweka mikakati na kufanya kazi kwa umoja ili kukabiliana na changamoto za umaskini na kuharakisha maendeleo ya Mkoa.
Akizungumza leo, Septemba 5, 2026, mara baada ya makabidhiano ya ofisi, Malima amesema Mkoa wa Lindi una fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumiwa ipasavyo zinaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo na kubadili maisha ya wananchi.
Amesema ni muhimu kwa watu wa Lindi kuwa na maamuzi na makubaliano ya pamoja kuhusu namna bora ya kutumia fursa zilizopo, hususan katika sekta za uwekezaji, kilimo, mifugo na maeneo mengine yenye uwepo wa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa.
“Lazima tukae tuamue na tukubaliana watu wa Lindi namna bora ya kukabiliana na umaskini. Tuanzishe mikakati ya pamoja itakayotuondoa hapa tulipo na kutupeleka kwenye maendeleo tunayoyataka,” amesema Mhe. Malima.

Aidha, amewataka viongozi kuwa wasimamizi wazuri wa fursa na rasilimali zilizopo katika maeneo yao, akisisitiza kuwa jukumu la Serikali si kutambua fursa pekee, bali kuhakikisha zinatumika kwa manufaa ya wananchi na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Katika kuimarisha kilimo, Malima ameagiza kila Halmashauri ya Mkoa wa hio kuhakikisha inapanda miche ya zao la korosho, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji na kuimarisha mchango wa kilimo katika uchumi wa Mkoa.
Pia, ametoa wito wa kuboresha fursa katika sekta ya mifugo na kuwataka viongozi kusimamia kwa karibu sekta hiyo ili wafugaji wawe sehemu ya mnyororo wa maendeleo, huku wakitumia shughuli zao za ufugaji kama fursa ya kiuchumi na kichocheo cha maendeleo ya Mkoa.
