Na Josea Sinkala, Mbeya.
Ubovu wa miundombinu ya barabara bado unaitesa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya (Jimbo la Mbeya vijijini) kutokana na ukubwa wa Halmashauri hiyo na ukubwa wa mtandao wa barabara unaochochewa na upatikanaji wa bajeti ndogo ya fedha kwa wakala wa barabara za vijijini (TARURA) wilayani Mbeya kutoka Serikali kuu.
Hayo yamedhihirika baada ya kaimu meneja wa TARURA wilayani Mbeya kuhitimisha kutoa taarifa yake ya utekelezaji wa miradi ya barabara za TARURA kwa hadi Disemba 2024, taarifa aliyoitoa kwa baraza la madiwani kwenye kikao cha robo ya pili ya mwaka 2024/2025 kilichofanyika Januari 29, 2025 wilayani Mbeya.
Kwa mujibu wa Mhandisi Arcad Tesha, kaimu meneja wa TARURA wilaya ya Mbeya mtandao wa barabara katika Halmashauri hiyo ni mkubwa lakini bajeti inayopokewa ni ndogo tofauti na uhalisia wa barabara katika jimbo la Mbeya vijijini.
TARURA inasema imejitahidi kuendelea kujenga barabara, madaraja na kufanya maboresho mbalimbali ya barabara lakini wamekuwa wakikabiliwa na kero mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti.
Naye kaimu meneja wa wakala wa ujenzi wa barabara Tanzania (TANROADs) mkoa wa Mbeya Mhandisi Nicodemus Kalenzo, amesema wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali na ipo kwenye hatua tofauti ikiwemo barabara ya Mbalizi Shigamba inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami kilomita 52 na tayari kilomita mbili zimepewa fedha ili kuanza utekelezaji kwani mkandarasi amekwishapatikana.
Aidha Mhandisi Kalenzo amesema barabara nyingine ambazo zipo kwenye mkakati ni ile ya Mbalizi Chang’ombe hadi Mkwajuni hadi Makongolosi na ile ya Isyonje Kikondo Makete ambayo inaendelea na ujenzi kutoka Makete mkoani Njombe kuja Mbeya na maombi yalishatumwa makao makuu ya TANROADs ili apatikane mkandarasi mwingine wa kuanzia mkoani Mbeya kwenda Makete.
Wakichangia kwenye eneo hilo la miundombinu ya barabara madiwani wameomba Serikali kuongeza jicho kwenye eneo la utoaji fedha kutokana na umuhimu wa miundombinu ya barabara hasa kwa Halmashauri ya Mbeya ambayo wananchi wake wengi ni wakulima hivyo kukwamishwa katika usafirishaji mazao yao.
Madiwani waliochangia kwenye kikao hicho wameeleza na mzigo walio nao TARURA lakini hawana fedha za kutosha kujenga barabara hizo za vijijini pamoja na madeni yanayoikabili TARURA kutokana na ufinyu wa bajeti pamoja na TANROADs kudaiwa na wakandarasi.