Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amewataka Waganga Wakuu wa Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha kuwa kadi za Bima ya Afya kwa Wote zinawafikia walengwa kwa wakati, sambamba na kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuelewa vizuri mpango huo.
Malima ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa zoezi la uandikishaji wa kaya zisizo na uwezo katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, awamu ya kwanza, ndani ya siku mia moja za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amesema kuwa jumla ya kaya 12,000 zenye zaidi ya watu 55,000 zinatarajiwa kunufaika na mpango huo ndani ya Mkoa wa Morogoro.

Kwa upande wake, Meneja wa Bima ya Afya Mkoa wa Morogoro, Mbala Shitindi, amesema kuwa awamu ya kwanza ya zoezi hilo inatarajiwa kunufaisha jumla ya kaya 931,000 zisizo na uwezo kote nchini.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Dkt. Michael Mbala, amesema utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote umerahisishwa kupitia ugawaji wa vifaa vya TEHAMA, hususan kompyuta, ambavyo vitasaidia katika zoezi la uhakiki na usimamizi wa wanufaika wa mpango huo.

Hafla ya uzinduzi huo iliambatana na zoezi la ugawaji wa kompyuta 21 na printa 6 kwa Halmashauri 8 zilizopo ndani ya Mkoa wa Morogoro, kwa ufadhili wa mpango wa Afya Yangu.