Na; mwandishi wetu
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umelaani vikali jaribio la kutekwa kwa Mwanaharakati na Mwanasheria Alphonce Lusako lililookea Desemba 05.2024 majira ya saa nne asubuhi, kwenye ofisi za “Reach Out Tanzania’ anapofanyia kazi, ofisi zilizopo Salmin Amour street, karibu na ofisi za Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Makumbusho, jijini Dar es Salaam
Taarifa ya THRDC iliyotolewa Desemba 05.2024 imeeleza kuwa Lusako alifika ofisini kwenye ofisi hizo, zilizopo kwenye wilaya ya Kinondoni majira ya saa nne asubuhi na ndipo watu wawili (mmoja wa kike na mwingine wa kiume) waliposogea kwenye gari yake mlango wa kulia, upande wa dereva huku mmoja kati yao akigonga mlango wa gari hiyo na kusema sisi ni Polisi tunakuhitaji, wakati huohuo upande mwingine kulikuwa na watu takribani 6 au 7 waliokuwa mbele ya jengo la ofisi yake
Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC Wakili Onesmo Olengurumwa imebainisha kuwa baada ya kuona hivyo, Lusako aliwahoji watu hao mnashida gani?, ndipo mmoja wao alipovuta mlango wa nguvu, huku yule wa kike akimuita Lusako kwa jina lake na kumsisitiza kuwa ashuke, na kwa vile watu hao wote walikuwa wamevaa nguo za kiraia na hawakumuonyesha vitambulisho inaelezwa alipata hofu hivyo alishuka na kuanza kukimbia akielekea kwenye geti la ofisini kwake huku akipiga kelele ‘natekwa, natekwa, nisaidieni’, na baada ya hapo Lusako alifanikiwa kuwatoroka watu hao
Hata hivyo, THRDC imeendelea kufafanua kuwa taarifa ya Jeshi la Polisi imeeleza kwamba Polisi walifika eneo hilo kwa nia ya kumkamata mtuhumiwa anayejulikana kwa jina la Emmanuel Mweta, lakini Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umefatilia tukio hilo na kwa mujibu wa Alphonce Lusako ofisini kwake hakuna mtu anayejulikana kwa jina la Emmanuel Mweta na kwamba askari hao walimwambia kuwa wanamuhitaji yeye Alphonce Lusako
THRDC imedai kuwa kuna taarifa ya kwamba Polisi hao waliondoka na begi la Lusako lenye laptop, pesa na mafaili ya kesi za wateja, hivyo kitendo cha kuondoka na gari la Lusako ilihali taarifa ya Polisi imeeleza kuwa walienda kumkamata Emmanuel Mweta zinaleta mkanganyiko zaidi juu ya taarifa iliyotolewa na Polisi, kufuatia kadhia hiyo:-
(i) Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kuheshimu sheria na kufuata taratibu za ukamataji kwa mujibu wa sheria ili kuepusha taharuki zisizo za lazima, Polisi wanapaswa kuvaa sare wakati wa ukamataji, kushirikisha uongozi wa serikali ya mtaa, kujitambulisha na kuonyesha vitambulisho vyao ili mtuhumiwa ajiridhishe kuwa ni kweli wakamataji ni askari Polisi
(ii) THRDC imetoa wito pia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunda ‘Tume Huru’ kwa ajili ya kuchunguza matukio ya utekwaji wa watu nchini na kwamba tume hiyo pia chunguze tuhuma za matukio ya utekwaji wa watu yaliyodaiwa kuwa vyombo vya dola vinahusika katika matukio hayo kwa namna moja au nyingine
Kuhusiana na hilo, mtandao huo umesema malalamiko hayo yamekuwepo kwa miaka mingi lakini hakuna chombo huru kilichoundwa kwa ajili ya kushughulikia masuala hayo ambayo yanachafua taswira ya nchi
(iii) THRDC imetoa wito kwa serikali kuridhia mkataba unaozuia masuala ya utesaji wa watu (Convention Against Torture -CAT) pamoja na mkataba wa Usalama wa Watu dhidi ya Utekaji na Upotezwaji wa Watu
(iv) Aidha, THRDC imetoa wito kwa viongozi wote nchini yaani kuanzia wa serikali, wa vyama vya siasa, wa tasisi za kidini na asasi za kiraia wajitokeze hadharani kukemea matukio hayo na wale wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia wachukue hatua kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambavyo amekuwa akihimiza
(v) THRDC pia, imetoa wito kwa Jeshi la Polisi kurudisha begi la Lusako lenye laptop, pesa na mafaili ya kesi za wateja wake mara moja.