Na; Raidhani Mohamedi
Jumatano ya Desemba 31, leo ndio siku ya mwisho kabisa ya mwaka 2025, zile hesabu za kwamba mwaka mmoja una siku 365 na robo au siku 366 basi hiyo siku ni leo, na ikimpendeza Mwenyezi Mungu itakapofika majira ya saa 06:00 usiku, Inshallah tutaanza kuhesabu siku ya kwanza kabisa ya mwaka mpya wa 2026, Inshallah
Mwaka mmoja ni muda mrefu sana wenye sekunde, saa, siku, wiki, na miezi, kwa kawaida ni kipindi chenye mambo mengi sana, tukianza kufanya tathmini na simulizi hapa kila mmoja anaweza kuja na kurasa lukuki za kitabu chake akieleza kumbukumbu alizonazo kwa mwaka huu, kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, familia, Kitongiji, Kijiji au Mtaa, Kata, Tarafa, Jimbo, Halmashauri au Wilaya, Mkoa hadi Taifa, na katika simulizi hizo pasi na shaka zipo kumbukumbu mbaya na nzuri, lakini zote hizo ni imani yetu kwamba zimetokea ili zikumbukwe na zitujengee tafakuri ya namna ya kuuendea mwaka ujao wa 2026
Siku chache zilizopita, Jambo TV ilikuletea simulizi ya makala inayoangazia matukio yaliyochukua nafasi na kutengeneza mijadala mikubwa Duniani, na kupitia simulizi ili tuliahidi kwamba tutaleta makala inayoangazia matukio yaliyochukua nafasi kwa mwaka huu (2025) yaliyotokea hapa nchini kwenye nyanja mbalimbali iwe siasa, jamii, uchumi, michezo, sanaa na burudani,
Kama nilivyoeleza hapo awali kila mmoja anaweza kuwa na kumbukumbu zake, na zote hizo zinapaswa kukumbukwa na kuheshimiwa lakini hapa tutaangazia zile tu tunazoona kwa namna moja au nyingine zilitikisa nchi, zikagusa hisia za wengi na pengine mjadala wake ulivuka mipaka ya Tanzania, Bara la Afrika na kujadiliwa pia kwenye maeneo mbalimbali Duniani,
Mwaka 2025 ambao hesabu zake zinafikia tamati hii leo, kama ilivyo kwa miaka mingine mingi iliyopita umekuwa na hekaheka nyingi, matukio yasiyofutika nk, hata hivyo jambo pekee ambalo nina uhakika usio na shaka kusema ni kwamba huenda huu ni mwaka utakaokuwa kwenye simulizi za wengi sana kutokana na matukio yaliyotokea kama tunavyoyachambua hapa kwa ufupi
(i) MATUKIO YA OKT. 29,
Kwa namna yoyote ile nitakuwa sijatenda sawa kama nitashindwa kuweka matukio yaliyotokea Oktoba 29 na siku zilizofuata namba moja, hii ni siku iliyokucha kawaida kabisa, utulivu usiokuwa wa kawaida ulishuhudiwa kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani kwenye Majiji makubwa kama vile Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Tanga, hadi Dodoma, kutoka Kusini hadi Kaskazini mwa Tanzania, Mashariki hadi Magharibi kote utulivu ulichukua nafasi yake, hii ni siku ambayo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ziliitangaza kuwa siku ya Uchaguzi Mkuu, Watanzania walikuwa na fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka watakaohudumu kwenye nafasi zao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo,
Lakini ni ukweli kwamba siku hiyo pia ndio iliyokuwa imepangwa kwaajili ya kile kilichoitwa kuwa ni maandamano ya amani, vuguvugu la maandamano haya lilianzia mitandaoni kwa takribani miezi miwili kabla, huku wanaharakati na wadau mbalimbali walioonesha kutokubaliana na uwepo wa uchaguzi wa huo wakidai kuwa ulikosa misingi ya haki, usawa na hivyo kushinikiza utawala wa sheria, waliendesha vuguvugu hilo, na ukweli baadaye ilikuja kubainika kuwa ushawishi wao ulipokelewa kwa hisia chanya
Licha ya Serikali na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vikiongozwa na Jeshi la Polisi kupiga marufuku uwepo wa maandamano hayo, lakini waratibu wake wa mitandaoni waliendelea kusukuma kete ya ushawishi wakishinikiza watu wajitokeze kwa wingi barabarani kuandamana, kwa namna iliyokuwa asubuhi ya Oktoba 29 hakuna aliyeamini kwamba mambo yangebadilika ndani ya saa chache baadaye
Binafsi nikiwa na wenzangu kadhaa tulikuwa mtaani kufuatilia mwenendo wa uchaguzi na muitikio wake, nilikumbuka kile nilichokiona pale Kimara mwisho mapema asubuhi na simulizi ya saa chache baadaye nashindwa kuamini hadi sasa kama ile ilikuwa ni Tanzania niliyoiona kwa miaka yote, kimsingi Watanzania walio wengi nikiwemo mimi sikufikiria kama maandamano hayo yatafanikiwa na hasa ikizingatiwa kuwa historia inaonesha wazi kuwa maandamano mengi yaliyoratibiwa kwa njia ile hapa nchini yamefeli mara nyingi iwe yameratibiwa na wanasiasa au Wanaharakati mtandaoni mwisho yaliangukia pua
Kutokana na sababu hizo za kihistoria, sikushangazwa hata nilipokuwa nasikia kauli za viongozi wa serikali, vyombo vya Dola, na wote waliokuwa wanapinga uwepo wa maandamano hayo, walipokuwa walisema kwamba waratibu wa jambo hilo mwisho wake watapata aibu ya karne kwakuwa watapuuzwa na Watanzania, lakini hapa ninaposimulia makala hii kila mmoja anajuwa kuwa mpaka sasa sio dhambi kusema kwamba tunaenda kuuaga mwaka huu na kuupokea mwaka mpya huku tukiwa tunaendelea kuuguza vidonda vya madhira ya Oktoba 29
Sina sababu ya kuadithia simulizi ambayo kila mmoja anaifahamu, lakini ili kuweka kumbukumbu sawa ya makala hii, Tanzania ilishuhudia mapito ambayo haijawahi kushuhudia katika historia yake, maandamano makubwa ambayo baadaye yalizaa vurugu yalishuhudiwa kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya, maneno ya Tunduma (Songwe), Tarime (Mara) nk, nayo yalipita kwenye joto la waandamanaji wengi wao wakiwa ni vijana (Gen Z)
Kufikia mchana kama sio jioni story haikuwa uchaguzi tena bali maandamano na waandamanaji, madhara ya vurugu yakajitokeza uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi ulishuhudiwa, majeruhi kutoweka kwa watu kwenye mazingira tatanishi na vifo vilivyoacha majeraha makubwa miongoni mwa Watanzania, ziko taarifa kwamba hadi sasa ziko familia zinatafuta wapendwa wao na pengine hawafahamu kama wapo hai au wamekufa
Madhira yaliyotokea Oktoba 29 mwaka huu na siku zilizofuata yaliendelea kushuhudiwa, kukamatwa kwa maelfu ya wananchi wake kwa waume, vijana kwa wazee wakihusishwa na ushawishi au kushiriki maandamano hayo yaliyozaa vurugu, wengi wao wakifunguliwa kesi kubwa kubwa zisizodhaminika kama vile uhaini, unyang’anyi wa kutumia silaha, uharibifu wa mali nk, licha ya kwamba maelfu ya wale waliokuwa wameshtakiwa kwa kesi hizo wameachiwa kwa dhamana au kufuatiwa mashtaka yao lakini ukweli ni kwamba bado kuna watu hadi sasa wapo kwenye kuta za magereza mbalimbali wakidaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine na vurugu hizo
Kando ya utitiri wa kesi zilizofunguliwa na Jamhuri kwenye maeneo mbalimbali nchini, lakini pia baadhi ya Watanzania na taasisi zisizo za kiserikali zimefungua kesi kadhaa dhidi ya Jamhuri wakiamini kwamba huenda madhira yaliyotokea Oktoba 29 mwaka huu na siku zilizofuata, pengine baadhi ya taasisi za serikali hazikutimiza majukumu yake kisawasawa
Miongoni mwa kesi hizo ni pamoja na ile iliyofunguliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) wakihoji uhalali wa tamko la IGP kuzuia watu kutotoka nje baada ya saa 12 jioni ikielezwa kuwa kutoa nafasi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi maalum, ipo kesi iliyofunguliwa na Mwanaharakati Rosemary Mwakitwange na wenzake wawili dhidi ya Wajumbe wote Nane (8) wanaounda Tume Huru ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati huo wakiongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TLS, wao wakidai kwamba Tume hiyo iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni batili na inakosa nguvu ya kisheria, sambamba na hilo ipo kesi iliyofunguliwa na kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakilalamikia kuzimwa kwa mtandao na kudorora kwa mawasiliano wakati wote huku watu wakiuawa, mali zikiharibiwa, na Taifa likiwa gizani
Ama kwa hakika kwenye mazingira ya kawaida ni ngumu kusimulia kumbukumbu za Oktoba 29 na siku zilizofuata, yapo mengi sana, suala la ripoti za vyombo vya habari vya kimataifa kama vile BBC, Al-Jazeera, VOA, na CNN, matamko ya Balozi na Jumuiya mbalimbali za kimataifa ambapo wengi wao wameonesha kulaani na kunyooshea kidole serikali ya Tanzania, hadi majibu ya serikali yaliyotolewa kwa nyakati tofauti kuanzia na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki chini ya Waziri Balozi Mahmoud Thabit Kombo, maelezo ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba hadi hotuba za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yote hayo bado hayajafunga mjadala Bali yamekoleza moto wa mjadala
Vipi kuhusu mjadala wa Bunge la Ulaya?, Je waandamanaji walilipwa?, Vipi kuhusu maisha ya Wanaharakati Watanzania wanaoishi nje ya nchi na ushirika wao na mabeberu?, Vipi kuhusu wivu wa raslimali zetu na njama ya kutaka kuipindua serikali, lakini umemsikia Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba?, hayo yote ni madhira yaliyotokea Oktoba 29 na siku zilizofuata, kwa hakika ilikuwa ni kipindi cha kihistoria
(ii) Matukio ya Utekaji na Kutoweka kwa watu kwenye mazingira tatanishi,
Naweza kusema hiki ni kiporo cha mambo yaliyojadiliwa na kulalamikiwa sana mwaka 2024 na miaka kadhaa iliyopita, watu wengi nikiwemo mimi tulidhani pengine mwaka huu (2025) mambo haya yangekuwa historia lakini imekuwa tofauti, bila kumung’unya maneno kwenye eneo hili hali imekuwa mbaya, na kwa hakika kupotea au kutoweka kwa mtu hata kwa mmoja tu haipaswi kuwa jambo la kawaida kamwe,
Yuko wapi Humphrey Polepole?, fikiria mtu aliyewahi kuwa Balozi wa Nchi Yetu kwenye mataifa ya Malawi na Cuba, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo na Mjumbe Wa Kamati Kuu CCM, Mkuu wa Wilaya mbalimbali nchini na Mjumbe wa Tume ya kukusanya maoni ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba leo hajulikani alipo, ametekwa na kutoweka kwenye mazingira tatanishi,

Umewahi kujiuliza kuhusu Mdude Nyagali?, Mwanaharakati na Kada wa CHADEMA mwenye makeke kutoka Nyada za Juu Kusini (Mbeya) leo hajulikani alipo, Vipi kuhusu Juma Kaswahili, lakini hatujawasahau mamia ya watu walioripotiwa kutekwa, kutoweka kwenye mazingira tatanishi na hata kuuawa, inawezekana wengine hawahusiani na mwaka huu (2025) lakini itakuwa dhambi kujadili au kuangaza jambo hili bila kuwakumbuka
Kuanzia Deus Soka, Ben Saanane, Azory Gwanda hadi mauaji ya Mzee Ali Kibao aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA makao makuu inasikitisha, kuna wakati Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilitoa orodha ya watu wanaodaiwa kutekwa, kutoweka kwenye mazingira tatanishi au kuuawa kwa miaka ya hivi karibuni, orodha hiyo ilikuwa na watu zaidi ya 100
Licha ya kwamba matukio mengi hayajathibitishwa na mamlaka husika hususani Jeshi la Polisi, hata hivyo mara kadhaa wamejitokeza na kutolea ufafanuzi kwenye baadhi ya matukio ya aina hiyo
Tunapouaga mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2026, ni wakati muafaka wa tafakuri pana kuhusu kukomeshwa kwa matukio ya aina hii, na pengine kupata majawabu ya kina kuhusu ndugu zetu waliotoweka kwenye mazingira tatanishi, kutekwa au kuuawa
(iii) UCHAGUZI NDANI YA CHADEMA, KESI YA UHAINI YA TUNDU LISSU, NA MAPITO YA CHADEMA
Katika ulingo wa siasa, mwanzoni kabisa mwa mwaka huu tulianza kushuhudia vuguvugu kubwa la mageuzi ndani ya Chama Kikuu cha Upinzani (CHADEMA -Chama cha Demokrasia na Maendeleo), kiuhalisia vuguvugu hilo lilianza tangu mwishoni mwa mwaka 2024 lakini uchaguzi na hitimisho lake limeshuhudia mwanzoni mwa mwaka huu

Katika hali isiyotarajiwa vita kali ya ndani na nje, makundi, kurushiana maneno na kukashfiana ilishuhudiwa miongoni mwa vigogo waliokuwa wanawania nafasi za juu kabisa za uongozi ndani ya chama hicho, Tundu Lissu aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara kabla alikuwa akichuana na aliyekuwa anatetea kiti chake kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe, Wajumbe wa Kamati Kuu John Heche aliyekuwa Mjumbe wa Kuteuliwa kabla alikuwa akipigana vikumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Viktoria ambaye sasa ametimkia chama tawala (CCM) Ezekia Wenje kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara
Unapotaja vita hii ya uchaguzi ndani ya CHADEMA kamwe huwezi kuacha kukumbuka namna watu mashuhuri kama vile Godbless Lema, Boniface Jacob (Boni Yai), Wakili Peter Madeleka, Emmanuel Ntobi na wengineo walivyokoleza moto na joto la uchaguzi huo, huku mijadala ya Chief Odemba nayo ikichukua nafasi, ama kwa hakika ilikuwa vita haswa
Wapo wanaodai kuwa, uchaguzi ule umebadili kila kitu kwenye siasa za CHADEMA na hata Tanzania kwa ujumla wake, kuingia madarakani kwa Tundu Lissu kama Mwenyekiti na John Heche kama Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara kumepokelewa kwa hisia mseto ndani na nje ya Tanzania
Wapo wanaaomini kuwa kuingia kwao kumeongeza mvuto zaidi kwenye chama hicho hasa vijana (Gen Z) na Wanaharakati ambao wengi walianza kutilia shaka mwelekeo wa CHADEMA chini ya Freeman Mbowe, kinyume chake wapo wanaaomini kuwa Lissu na Heche ni kama wamekuja kukiua chama wakidai kwamba wamekuwa wakitanguliza harakati badala ya siasa,
Sipo hapa kueleza upande gani upo sahihi au la kutokana na mitazamo hiyo, lakini ninachoweza kusema ni kwamba kitendo cha Freeman Mbowe kushindwa dhidi ya Tundu Lissu na Wenje kushindwa dhidi ya Heche kwenye uchaguzi ule, ilikuwa ni mwanzo wa maisha mapya kabisa ya siasa za CHADEMA na Tanzania kwa ujumla wake, misimamo yao, kukubalika kwao miongoni mwa jamii, kuendesha siasa harakati nk ni miongoni mwa mambo yaliyowabeba zaidi kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi huo
Waliingia madarakani wakipokea kijiti cha kampeni ya ‘No Reforms, No Election’, ilichukuliwa kama kauli mbiu ya kawaida tu lakini ‘jamaa’ wakaanza kwa kuutangazia umma kuwa wamejipanga kuzuia uchaguzi endapo mabadiliko ya msingi waliyokuwa wanadai yasingefanyika,
Vikao vya ndani ya chama, vikao vya siri na wadau mbalimbali kama vile Jaji Joseph Sinde Warioba, Mzee Butiku na hata Marehemu Raila Odinga wa Kenya walikutananao kueleza namna watakavyosimamia kampeni yao hiyo, mikutano ya kuzunguka nchi nzima ilifuata, Kanda ya Nyasa, Kati, Magharibi, Viktoria, Serengeti, Pwani, Unguja, Pemba hadi Kusini mwa Tanzania kote walilenga kufika, lengo kueneza ‘No Reforms, No Election’ kwa umma wa Watanzania
Mpango sio matumizi akiwa Kusini mwa Tanzania (Mbinga, mkoani Ruvuma) Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Tundu Lissu alikamatwa na maafisa wa Jeshi la Polisi mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu kabla ya baadaye kusafirishwa hadi Dar es Salaam na kisha kufunguliwa kesi ya uhaini inayoendelea kumuweka gerezani hadi sasa kwakuwa haina dhamana,
Wakati ukidhani story za CHADEMA zimefika mwisho, jamaa waliwashangaza wengi walipotangaza kuendelea na oparesheni hiyo, safari hii Katibu Mkuu John Mnyika akivua suti za Ofisini na kuongeza nguvu majukwaani, misafara miwili ya nguvu ya Heche na Mnyika ilishambulia maneno mbalimbali nchini kama vilevile iliyokuwa kwa Lissu na Heche, jamaa waliendelea kunadi sera, misimamo ya chama chao kuelekea uchaguzi mkuu kupitia oparesheni ‘No Reforms, No Election’
Ilipokelewaje?, wangezuiaje uchaguzi?, haya ni miongoni mwa maswali yaliyosumbua wengi lakini wakati tukisubiri majibu yake, huku Lissu akiwa ndani ghafla aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar Said Issa Mohamed na wenzake wawili wanafungua kesi ya madai, wakidai kwamba chama hicho kinaitenga Zanzibar kwenye mgawanyo wa mali, raslimali fedha nk, wanaenda mbali zaidi na kueleza kwamba viongozi wa chama hicho wamekuwa wakitoa kauli zinazohatarisha Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika (Tanzania Bara) na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia wanadai kwamba kumekuwa na ubaguzi wa kijinsia ndani ya chama hicho
Pamoja na hoja zote hizo, Said Issa Mohamed na wenzake wanaiomba Mahakama kuzuia shughuli zote za kisiasa na kiutendaji ndani ya CHADEMA hadi hapo kesi ya msingi itakaposikilizwa, Mahakama inakubali maombi yao, CHADEMA na viongozi wake wanazuiliwa, na hapo Oparesheni ‘No Reforms, No Election’ inakuwa njia panda
Wakati upande wa pili Lissu akichukua hatamu ya kujitetea mwenyewe, kesi ikirushwa mubashara na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwenye Mahakama ya ukabidhi pale Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam -Kisutu, wakati jambo hilo la kihistoria likiendelea na maelfu wakifuatilia kesi hiyo mubashara kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ghafla Said Issa Mohamed na wenzake wanafungua kesi nyingine Mahakama Kuu wakidai kuwa viongozi waandamizi wa CHADEMA wakiongozwa na Heche wamedharau amri ya Mahakama, Mahakama inasikiliza na kutupilia mbali hoja hiyo
Kwingineko, Msajili wa Vyama vya Siasa anapokea malalamiko ya Kada wa chama hicho Lembrose Mchome na ajenda ya akidi kwenye mkutano wa Baraza Kuu, sakata hilo linapelekea Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutangaza kutowatambua viongozi wote walioteuliwa na kuthitishwa na Baraza Kuu la CHADEMA lililofanyika mwanzoni mwa mwaka huu, Katibu Mkuu John Mnyika na Manaibu wake wawili Amani Golugwa na Wakili Ali Ibrahim sambamba na Wajumbe wa Kamati Kuu wa Kuteuliwa wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Dkt. Rugemeleza Nshala, inaonekana hawana nguvu ya kisheria kuendelea na majukumu yao, CHADEMA inaamua kuwakaimisha na miezi michache baadaye Mahakama Kuu Kanda ya Manyara inawarejeshea ‘hadhi’ yao, kiufupi umekuwa mwaka wa CHADEMA na Mahakamani, hapo sijazungumzia mamia ya makada wao waliokamatwa, kushikiliwa na pengine kufikishwa Mahakamani wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali, ingawa hakuna uthibitisho wa moja kwa moja wapo wanaaomini kwamba huenda maandamano yaliyozaa vurugu za Oktoba 29 inawezekana kwa namna moja au nyingine yalitokana na hamasa ya Oparesheni ‘No Reforms, No Election’
Kuna simulizi kubwa inayohusu maisha ya CHADEMA kwa mwaka 2025, unaikumbuka CHAUMMA?, ndio nazungumzia Chama cha Ukombozi wa Umma, wazee wa sera ya Ubwabwa chini ya Mzee wangu Hashim Rungwe Spunda, makada wengi wa CHADEMA wakiwemo waliokuwa Wajumbe wa Kamati Kuu, Baraza Kuu, Mkutano Mkuu, Mabaraza ya Vijana, Wanawake, Wazee na mamia kwa maelfu ya wanachama wa kawaida walitangaza kukihama chama hicho na kukimbilia CHAUMMA, madai yakiwa ni kwamba hawakubaliani na mpango wa chama chao cha zamani wa kuamua ‘kugomea’ uchaguzi kutokana na kwamba mabadiliko wanayodai hayajafikiwa, wakakimbilia kwa Mzee Rungwe kwenda kushiriki uchaguzi, angalau wamepata Mbunge mmoja wa jimbo na wawili wa Viti Maalum, CHADEMA imefanikiwa au imefeli?, jibu linabaki kwako
(iv) UCHAGUZI MKUU,
Awali katika makala hii nimeeleza namna matukio ya Oktoba 29 (Siku ya Uchaguzi Mkuu) yalivyoacha historia ya kipekee, lakini hapa tuangazie namna mchakato wa Uchaguzi Mkuu ulivyokuwa hadi matokeo yake kutangazwa, kuapishwa kwa washindi na maoni mseto ya mchakato huo

Kama ilivyo kawaida, inaeleweka kwamba kila baada ya miaka mitano (5) Nchi yetu inaingia kwenye zoezi hilo muhimu kabisa la kisheria na Kikatiba, hata hivyo uchaguzi wa mwaka 2025 umekuwa wa kipekee kutokana na misimamo na migongano ya mapema kabisa ya wadau wa siasa, wengi wakiamini kwamba kwa mara ya kwaza Tanzania imeingia kwenye uchaguzi mkuu huku wadau wa siasa wakiwa hawakubaliani namna ya kuuendea uchaguzi huo
Kwa mara ya kwanza katika historia yake Nchi yetu tumeshuhudia ikiingia kwenye uchaguzi mkuu huku Chama Kikuu cha Upinzani kikiwa kimegomea kushiriki, CHADEMA wao walikuwa wanatilia mkazo kampeni yao ya ‘No Reforms, No Election’ na ilidhihirisha wazi kuwa hawatashiriki uchaguzi pale walipogomea kusaini kanuni za kuendesha uchaguzi huo, INEC ikatangaza kuwa chama hicho hakina sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu au chaguzi ndogo zitakazofuata hadi mwaka 2030, ACT Wazalendo chama cha pili kwa ukubwa kwenye upande wa upinzani na Chama Kikuu cha Upinzani upande wa Zanzibar wao wakasema wanaingia kwenye uchaguzi lakini wakaja na kauli mbiu isemayo ‘Tunapambana Tukishiriki, Tunashiriki Tukipambana’ Muhuni Hasusiwi’, unaweza kujiuliza muhuni ni nani?, nikuambie tu hata Mimi simjuwi, CCM kama chama tawala wao wakasema ‘Oktoba Tunatiki’
Kauli mbiu hizi za vyama vitatu vikubwa hapa nchini zinaonesha wazi kuwa uchaguzi wa mwaka huu tumeingia Taifa likiwa kwenye mgawanyiko, hadi nasimulia makala hii sijuwi mgawanyiko huo tunaweza kuumaliza kwa njia gani?, lakini jambo moja ninaloweza kusema ni kwamba sote tujuwe tuna Tanzania ya kuijenga na kuilinda
Kando ya CHADEMA, ACT Wazalendo ndio iliyotarajiwa kuwa mshindani wa karibu wa CCM kwenye uchaguzi mkuu hasa kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kitendo cha mgombea aliyekuwa ameteuliwa na chama hicho Luhaga Mpina aliyehamia akitokea CCM kuenguliwa kiliacha maswali lukuki na mjadala mpana kuhusu mustakabali wa siasa za ushindani na vyama vingi nchini,
Kwenye eneo hilo pia hatuwezi kuacha kugusia baadhi ya mambo yaliyotokea ndani ya CCM na serikali ambayo kimsingi yaliacha midomo wazi na mjadala sio tu Tanzania bali hata nje ya nchi
Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa zamani wa jimbo la Ruangwa, mkoani Lindi, tangazo lake la kuamua kutogombea Ubunge liliwastua wengi, tena ikizingatiwa kuwa ndani ya majuma mawili tu nyuma aliutangazia umma kuwa anarudi tena kwenye kinyang’anyiro hicho, alisubiri hadi siku ya mwisho ya mchakato wa ndani ya CCM wa uchukuaji fomu kutangaza maamuzi hayo yaliyoacha maswali hadi sasa

Dkt. Tulia Ackson, Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini (zamani) sasa akiwa Mbunge wa jimbo la Uyole, mkoani Mbeya, Spika Mstaafu na Rais wa Umoja wa Mabungw Duniani (IPU) anayemaliza muda wake, naye uamuzi wake wa kujiengua kugombea kiti cha Spika yaani kutetea nafasi yake kiliacha watu midomo wazi na hadi sasa bado wengine wana maswali, ikizingatiwa kuwa alichukua fomu ndani ya chama chake na alikuwa mmoja wa makada wa tatu waliokuwa wamepitishwa na Kamati Kuu kupigiwa kura na Wabunge wateule wa CCM, lakini dakika za mwisho akatangaza kujiondoa

Jambo lingine ambalo kimsingi ni la kawaida, lakini kiuhalisia limeacha midomo ya watu wengi wazi na maswali lukuki ni pamoja na Baraza jipya la Mawaziri lililotangazwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni, kuachwa kwa Mbunge wa Bukombe na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko, Hussein Bashe (Mbunge wa Nzega Mjini na aliyekuwa Waziri wa Kilimo), Innocent Bashungwa (Mbunge wa Karagwe na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi) na wengineo kumeacha maswali lukuki pia, ikizingatiwa kuwa hao ni miongoni mwa Mawaziri walioonekana kuwa vipenzi kweli kweli vya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
(v) MENGINEYO,
Kama nilivyoeleza mwanzoni mwa makala hii kuwa kuna mambo mengi sana yametokea kwa mwaka huu (2025) kwenye nyaja zote za siasa, jamii, uchumi, michezo, sanaa na burudani, na kwa namna yoyote ile ni ngumu kuweza kusimulia hapa, hata hivyo hatuwezi kuyataja mengine kwa uchache yaliyokuwa yamechukua nafasi na kutengeneza mijadala mikubwa ndani na nje ya nchi
Sakata la kufungiwa hadi kufunguliwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo chini ya Askofu Dkt. Josephat Gwajima, Misiba ya vigogo iliyotokea mwaka huu kama vile kifo cha Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa David Msuya, kifo cha karibuni cha aliyekuwa Mbunge wa Peramiho na Waziri Mwandamizi kwenye Wizara mbalimbali Jenista Mhagama, Misukosuko ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) iliyokuwa inaundwa na vyama vya CCM na ACT Wazalendo ambayo pia hadi wakati huu iko njia panda, ongezeko la ajali za Barabarani na kasi ya matumizi ya mitandao ya kijamii kwa vijana (Gen Z) ni miongoni mwa mambo yaliyochomoza sana mwaka huu (2025),
Wadau wa Michezo pia wanaweza kusema kusema huu umekuwa mwaka wa baraka kwenye sekta hiyo, pamoja na mambo mengine Michuano ya CHAN 2024 iliyofanyika mwaka huu 2025 ikiandaliwa kwa pamoja na mataifa ya Afrika Mashariki (Tanzania, Kenya na Uganda) kwa mara ya kwanza imeshuhudiwa Timu ya Taifa ya Tanzania ikitinga hatua ya robo fainali, lakini kama hiyo haitoshi ni jana tu katika historia Taifa Stars imetinga hatua ya 16 bora ya Michuano ya AFCON inayoendelea kutimua vumbi nchini Morocco, kila la kheri kwa Taifa Stars na Tanzania kwa ujumla wake.
Ahsante 2025, karibu 2026.