Latest Posts

MNADA WA KWANZA WA KITAIFA WA KOROSHO WAFANYIKA TANDAHIMBA, ZAIDI YA TANI 26,000 ZAUZWA

Mnada wa kwanza wa Kitaifa wa zao la korosho kwa msimu wa 2024/2025 umefanyika leo, Novemba 8, 2025, ambapo zaidi ya tani 26,000 zimeuzwa kwa bei ya juu ya Sh 3,520 na bei ya chini ya Sh 2,550 kwa kilo.

Mnada huo umefanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara kupitia Chama Kikuu cha Ushirika kinachohudumia Newala na Tandahimba (TANECU).

Akizungumza wakati wa mnada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Michael Mntenjele, amewataka wakulima wa korosho kuhakikisha wanaendelea kuzitunza korosho zao ili ziendelee kuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya soko.

Amesema lengo ni kuhakikisha wakulima wanazalisha korosho zenye ubora wa kuvutia wanunuzi kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Kanali Mntenjele amesema Tanzania imeendelea kufanya vizuri ikilinganishwa na nchi nyingine zinazozalisha korosho kama Msumbiji, Brazil, Zambia na Kenya, kutokana na kuuza korosho zenye ubora wa hali ya juu na kwa bei shindani kimataifa.

“Hali hii inatokana na ubora wa korosho zetu, ladha nzuri, pamoja na mfumo madhubuti wa udhibiti ubora wa korosho zinazoingia sokoni,” amesema.

Aidha, ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya ushirika (AMCOS) na waendesha maghala kuwa waaminifu na wazalendo kwa kuepuka kupokea korosho chafu au kuchanganya na vitu visivyo korosho.

“Kwa kufanya hivyo, wakulima watapata malipo yanayoakisi jasho lao na tutaendelea kuvutia wanunuzi wengi wa ndani na nje ya nchi zaidi ya hapo, tutaendelea kulinda hadhi na sifa ya korosho ya Tanzania inayotambulika duniani.”, Amesisitiza Mntenjele.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred amesema ili kukabiliana na changamoto za hali ya hewa hususani mvua zinazoendelea katika maeneo mbalimbali, pamoja na kupunguza mlundikano wa korosho ghafi katika ghala kuu, bodi hiyo imetoa ruhusa ya kusafirisha korosho ghafi kwa saa 24 kutoka ghala kuu kwenda Bandari ya Mtwara au katika ghala za wanunuzi.

Ameeleza kuwa ruhusa hiyo inahusu mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, ambapo korosho zitasafirishwa moja kwa moja kwenda bandari ya Mtwara kwa ajili ya usafirishaji.

Nao baadhi ya wakulima wameiomba serikali na wadau wa korosho kuangalia namna ya kuongeza bei ya zao hilo, wakieleza kuwa gharama za uzalishaji ni kubwaft ukilinganisha na mapato wanayopata kutokana na bei iliyopo sokoni, licha ya baadhi ya korosho kufikia bei ya juu ya Sh 3,520.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!