Timu 18 zinatarajiwa kushiriki ligi ya Mtenga Jimbo Cup Season 2 (awamu ya pili) katika jimbo la Mtwara mjini Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Akizungumza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mtwara, Salumu Naida wakati wa kukabidhi jezi kwa viongozi wa timu shiriki wa timu hiyo amesema viongozi hao wafuate utaratibu, kusimamia maadili ya michezo pamoja na kuendeleza uzalendo wa Mtwara ili kutimiza lengo la kuwaunganisha wakazi wa mkoa huo.
Lengo la ligi hiyo ni kuwaunganisha watu na isiwe sababu ya kufarakanisha watu hivyo watumie fursa hiyo kuhamasishana kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura na kujitokeza kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini Hassan Mtenga amesema kuwa ligi hiyo ni muendelezo wa kuunga mkono juhudi za Rais wa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika michezo.
Imeelezwa kuwa kipindi chote cha mashindano hayo kutakuwa na timu ya watu 14 ambao wanasaka vipaji kwenye mashindano hayo.
“Lengo la kufanya hivyo ni kuona namna ya kuwasaidia vijana hao ili wazidi kukua kwenye soka na kuonekana na wadau wa soka” Amesema Mtenga.
Zuber Zuber, mdau wa mpira wa miguu mkoani Mtwara amempongeza mbunge huyo kwa kitendo anachofanya kwa kuanziasha ligi hiyo kwani miaka ya hivi karibuni Mtwara kumekosekana muamko wa mchezo wa mpira wa miguu ukilinganisha na kipindi cha miaka ya nyuma.
Mashindano hayo yatahusisha timu kutoka kila kata ndani ya manispaa hiyo ambapo mshindi wa kwanza atapata kiasi cha Shilingi milioni 1, wa pili Shilingi laki 5 na wa tatu atajinyakulia Shilingi laki 3.
Mashindano ya mpira wa miguu yaliyoanzishwa na mbunge huyo mwaka huu ni ya awamu ya pili na takribani timu 18 zinatarajia kushiriki ligi hiyo ambapo mechi ya ufunguzi itafanyika Julai 13, mwaka huu katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.