Mkoa wa Morogoro umejipanga kikamilifu katika kuhakikisha utunzaji wa mazingira unaendelea kwa kupanda miche mbalimbali milioni 30 ikiwemo karafuu, jambo litakaloenda kuongeza uoto wa asili na kutunza mazingira hususan maeneo ya milimani.
Hayo yamebainishwa leo Januari 27, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati akifanya zoezi la kugawa na kupanda miche katika Shule ya Msingi Juhudi, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, ikiwa ni katika kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kusheherekea siku yake ya kuzaliwa.

Malima amesema kuwa Mkoa wa Morogoro unakabiliwa na changamoto ya wakazi wake kukata miti ovyo jambo linalopelekea kukauka kwa vyanzo vya maji. Hivyo, zoezi la upandaji wa miche mbalimbali milioni 30 ikiwemo miche ya karafuu litaenda kuongeza chachu ya utunzaji wa mazingira kwa maslahi mapana ya Wanamorogoro na taifa kwa ujumla.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika mkoa huo watachagiza upandaji wa miche.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Morogoro–Rufiji (NEMC), Bw. Arnold Mapinduzi amesema kuwa katika kuungana na Rais kufurahia siku yake ya kuzaliwa, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kuhakikisha wanatunza na kuhifadhi mazingira ambapo utunzaji wa mazingira unaendana na upandaji wa miti.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Bw. Emmanuel Mkongo, amesema kuwa kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, kila Mtanzania akiweza kupanda mti mmoja atakuwa amechangia kwa asilimia kubwa kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
