Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mwalimu Hassan Nyange, ameonesha kutoridhishwa na matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2025, ambapo manispaa hiyo imefaulisha kwa asilimia 84.1.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wakuu wa shule, walimu wa shule za msingi na waratibu elimu kata kwa ajili ya kufanya tathmini ya matokeo hayo, kilichofanyika Novemba 7, 2025 katika Chuo cha Ualimu Kawaida Mtwara (TTC), Mwalimu Nyange amesema lengo la kikao hicho ni kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza ufaulu katika mwaka ujao.

Amesema bado kuna changamoto ya walimu kutojitathmini ipasavyo, na hivyo amewataka kusimamia kwa umakini elimu ya watoto ili kuwasaidia kuwa na mwelekeo bora wa maisha yao ya baadaye.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuongeza bidii katika ufundishaji na kushirikiana kwa karibu ili kuendelea kuipandisha hadhi ya Manispaa hiyo katika matokeo ya kitaifa.
Pamoja na kutoa maonyo na maagizo hayo, Mwalimu Nyange hakusita kuwapongeza walimu kwa jitihada walizoonyesha ambazo zimewezesha manispaa hiyo kufanya vizuri kwa kiwango cha kuridhisha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewataka walimu wa idara ya elimu msingi kushirikiana katika mipango na mikakati ya kuinua ufaulu, huku akisisitiza umuhimu wa kuwajenga wanafunzi katika kuona elimu kama kipaumbele cha kwanza katika maisha yao.
Mwaipaya amesema ushirikiano kati ya walimu, wazazi na viongozi wa elimu ni muhimu katika kuhakikisha ustawi wa elimu unazidi kuimarika na kizazi cha Mtwara kinapata msingi bora wa maendeleo.