Monicka Ndungulu, mkazi wa Kata ya Mji Mwema katika Halmashauri ya Mji wa Njombe na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema kwamba licha ya chama chake kutojihusisha na uchaguzi, wananchi wa kata hiyo wanapaswa kuchagua kiongozi mwenye maono badala ya kuangalia itikadi za vyama.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia ACT Wazalendo, Abuu Mtamike, Monicka amesema ameamua kumtetea mgombea huyo kwa kuwa amerudishwa rasmi baada ya kushinda rufaa dhidi ya pingamizi lililowekwa na mgombea wa CCM.
“Hatuendi kwa ajili ya chama. Mimi ni No Reform, No Election, lakini kwa sababu jembe hili limerudi, mpeni kura. Sisi ni wananchi maskini sana, tunahitaji mtu atakayetusemea,” amesema Monicka.
Kwa upande wake, Mtamike amesema sababu kuu ya kuwania nafasi hiyo ni kupigania maslahi ya wananchi wa kata hiyo, akisisitiza kwamba hawezi kukaa kimya wakati wananchi wakiteseka kutokana na uongozi mbovu uliopo madarakani