Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Rehema Mlawa, ameongoza mkutano mkuu wa jumuiya hiyo na kusimamia upigaji wa kura za maoni kwa ajili ya kupata wagombea wa viti maalum vya udiwani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Shule ya Wasichana ya Bibi Titi, makao makuu ya Wilaya ya Rufiji, Utete, na kuratibiwa na Katibu wa UWT wilayani humo, Mariam Mugasha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mwenyekiti Rehema Mlawa amewataka wajumbe wa mkutano huo kufanya maamuzi yenye busara kwa kuchagua viongozi wenye sifa, uwezo na maadili ya kuwatetea wanawake katika halmashauri ya wilaya.
Wajumbe wa mkutano huo pia walitumia fursa hiyo kupongeza utekelezaji wa Ilani ya CCM katika nyanja mbalimbali wilayani Rufiji, wakielezea kuridhishwa na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais na Mwenyekiti wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maeneo yaliyotajwa kuwa yamepiga hatua kubwa ni pamoja na sekta ya elimu, afya, na miundombinu ya barabara, ambayo imekuwa ikipitika muda wote na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, wajumbe hao walieleza dhamira yao ya kujitokeza kwa wingi kupiga kura mwezi Oktoba mwaka huu, wakiahidi kumpigia kura Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kuwa ataendeleza kasi ya maendeleo nchini.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Rufiji, Frederick Msae, amewataka wajumbe wa mkutano huo kujiepusha na vitendo vya rushwa, akisisitiza kuwa mgombea anayetumia rushwa hafai kuchaguliwa kuwa kiongozi.