Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo Othman Masoud Othman (OMO) amesema miongoni mwa sababu zilizomsukuma kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hiyo ni uwepo wa mambo mengi ya msingi ambayo yanahitajika kurekebishwa kwa haraka Zanzibar
Akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari Serena Hotel, jijini Dar es Salaam leo, Jumamosi Agosti 23.2025 OMO ametaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na mfumo wa Muungano, uchumi wa Zanzibar, mfumo wa uwajibikaji, utendaji wa vyombo vya utoaji haki, utumishi wa umma, utawala mwema, na mfumo mzima wa usimamizi wa ardhi uwezeshaji kiuchumi
Mengine ni uwezeshaji wananchi katika maisha, mustakabali wa urithi wa Zanzibar, huduma za kijamii na matumizi ya teknolojia ambapo amesema yeye binafsi anaamini taaluma, uzoefu, imani na dhamira yake ya dhati kwamba Zanzibar inahitaji mageuzi makubwa ili ipate maendeleo endelevu, ustawi wa kijamii, amani na utulivu wa kudumu
“Huu ni uwanja mpana ambao tunaweza leo hii kuutendea haki kwa kubadilishana mawazo, kupeana ufafanuzi wa mambo kadhaa ambayo mtakuwa na haja ya kupata ufafanuzi na kupeana rai na mawazo juu ya namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika maeneo hayo” -OMO
OMO ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Taifa na Makamu wa Kwanza wa Rais SMZ amesema chama hicho kimeuita uchaguzi wa mwaka huu (2025) kuwa ni uchaguzi wa maamuzi na kwamba ni mwaka wa kuinusuru Zanzibar
“Chama chetu kilianza msimu huu wa siasa kwa kuandaa ahadi ya chama kwa Watanzania (Brand Promise) kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ahadi ya chama pamoja na tafiti zilizofanyika katika masuala mbalimbali yalitupelekea kuandaa ilani za pande zote mbili za muungano, tutainadi ilani yetu na tutajenga hoja yetu” -OMO.
Akizungumzia sababu zilizopelekea chama hicho kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu (2025) OMO amesema ziko fursa walizoziona kabla ya kuchukua maamuzi hayo ikiwemo kutoa mwanya kwa wananchi kutambua ‘mabaya’ yanayofanywa na ‘watawala’ na ‘Tume’ licha ya kwamba wanatambua kuwa mazingira ya kuelekea uchaguzi huo kwa pande zote mbili za muungano si rafiki sana
Katika hatua nyingine, akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa Wahariri hao OMO amesema chama hicho kitatoa taarifa rasmi hivi karibuni kuhusiana na sakata lililoibuliwa na kada wake Monalisa Ndala (Mwenezi wa ACT Wazalendo mkoa wa Dar es Salaam) anayedai kuwa mchakato wa kumpata mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa chama hicho Luhaga Mpina umekengeuka misingi ya kikatiba na kikanuni ya chama hicho, ambapo licha ya kwamba taarifa rasmi itatolewa lakini amesema wao kama chama wanaamini mchakato huo ulikwenda sawa na hakuna sehemu yoyote iliyokengeukwa.