Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo pamoja na wadau wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho ya nanenane, akisisitiza kuwa ni jukwaa muhimu la kupata maarifa, teknolojia na mbinu za kisasa zitakazosaidia kuongeza tija na kukuza uchumi.
Malima ametoa wito huo Agosti 7, 2025, alipowatembelea wadau wa kilimo ufugaji na uvuvi kuelekea kilele cha kufunga maadhimisho hayo ambapo amesema ushiriki wa wananchi katika maonesho hayo unatoa fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu na taasisi mbalimbali zinazoshiriki, hivyo kuchochea mabadiliko chanya kwenye sekta hizo ambazo ni mhimili mkubwa wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Naomba nitumie nafasi hii kuwasihi wananchi wa Morogoro na maeneo ya jirani kutumia muda huu uliosalia kujitokeza kwa wingi hapa viwanjani,kupata maarifa, teknolojia, na mbinu nyingi za kisasa zinazoweza kubadili maisha ya wakulima wetu, wafugaji, na wavuvi,tusikose fursa hii ya kipekee,” Malima.
Aidha, Malima ameongeza kuwa maadhimisho ya nanenane ni zaidi ya maonesho ya bidhaa na huduma kwani ni jukwaa la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kukuza ushirikiano kati ya sekta binafsi, serikali na wananchi kwa ujumla pia amewapongeza washiriki wote waliotoa mchango wao katika maonesho hayo na kuwataka kuendeleza uhusiano mzuri uliopatikana hapo viwanjani.

Malima amesisitiza umuhimu wa kutumia maarifa yanayopatikana katika maonesho hayo kuwafikia wakulima waliopo vijijini, ili kile kinachofundishwa kiweze kuleta tija katika uzalishaji na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Katika maadhimisho hayo ya mwaka huu, kaulimbiu inasema: *“Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, 2025.