Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani, amesema kuwa ili sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ziwe na tija kwa taifa, ni lazima zisimamiwe na viongozi bora, wenye dira na weledi wa kutosha kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
Akizungumza Agosti 8, 2025, katika kilele cha Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika katika Viwanja vya Julius K. Nyerere mkoani Morogoro, Batilda amesema viongozi bora ni kiungo muhimu kati ya wananchi na maendeleo ya kisekta.
“Hatutoweza kupata tija katika sekta hizi muhimu pasipo kuwa na viongozi bora,ni wajibu wetu kuhakikisha tunawachagua na kuwaweka viongozi sahihi, ili kukuza sekta hizi na hatimaye kuimarisha uchumi wa taifa letu,” amesema Balozi Batilda.

Aidha, amesisitiza kuwa maonesho ya nanenane hayapaswi kuchukuliwa kwa wepesi, bali yaendelezwe kisasa kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuyaboresha ili kuongeza ufanisi na kuvutia wadau wengi zaidi,Pia ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi na kuongeza fursa za mafunzo kwa vitendo kwa vijana na wakulima kupitia Halmashauri nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema maonesho ya mwaka huu yameandika historia mpya kwa kuwa na zaidi ya washiriki 11,200 huku zaidi ya wananchi 100,000 wakitembelea maonesho hayo hadi kufikia kilele chake.

Amesisitiza kuwa mafanikio hayo hayapaswi kubaki viwanjani pekee, bali ni wajibu wa viongozi na watendaji kuyapeleka maarifa na teknolojia zilizotolewa katika maonesho hayo kwa wananchi wa vijijini ili yaweze kuwa na tija katika maisha yao.
Naye Mwakilishi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro Zangina Shanang amesema kuwa chama hicho kimeridhishwa na namna maonesho ya mwaka huu yalivyoandaliwa, kufanikishwa na kushirikisha wadau wengi, ikiwa ni ishara ya mshikamano na ustawi wa sekta ya kilimo na uchumi kwa ujumla.
