Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa Serikali ya Tanzania katika ziara ya kimkakati jijini Lagos, Nigeria, kutembelea Kampuni za Dangote.
Katika ziara hiyo, Prof. Kitila amefanya mazungumzo ya kimkakati na Rais na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaj. Aliko Dangote kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa uwekezaji kati ya Tanzania na kampuni hiyo kubwa zaidi ya viwanda barani Afrika.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa kutafsiri maono ya Dira 2050 ambayo imesema Sekta Binafsi ndiyo iwe injini ya kujenga uchumi katika safari ya kulifikia taifa lanye uchumi wa Dola za Marekani Trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Pia ziara hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano unaozidi kuimarika kati ya Serikali ya Tanzania na Dangote Group, kutokana na ziara ya hivi karibuni ya Alhaj Dangote nchini Tanzania ambapo alikutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kufanya mazungumzo kuhusu kupanua uwekezaji katika sekta mbalimbali za kimkakati za uchumi.
Mazungumzo hayo yaliweka msingi wa kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na kuharakisha maendeleo ya viwanda nchini Tanzania huku ziara ya Lagos ikiwa ni hatua inayofuata ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa Dar es Salaam kupitia miradi ya uwekezaji na ushirikiano wa muda mrefu.

Mbali na Prof. Kitila Mkumbo, ujumbe huo unajumuisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga; Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba; Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile; Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya.
Wengine ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa; Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Balozi Dkt. Aziz Mlima; Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gillard Teri; viongozi wandamizi serikalini na watengaji wakuu wa mashirika mbalimbali ya kwenye sekta za uchukuzi, usafirishaji, ugavi, bandari na miundombinu
Akizungumza wakati wa kikao hicho Alhaji Dangote amempongeza Rais Dkt. Samia kwa uongozi wake wenye maono na jitihada za kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Amesema mageuzi yanayoendelea kutekelezwa chini ya uongozi wake yameongeza imani ya wawekezaji, kuboresha urahisi wa kufanya biashara na kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi zinazovutia zaidi uwekezaji wa kimkakati barani Afrika.
Alhaji Dangote amesema kuwa mazungumzo aliyofanya na Rais Samia wakati wa ziara yake nchini Tanzania yameimarisha zaidi imani ya Dangote Group katika mwelekeo wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
Ameeleza kuwa Tanzania ina fursa kubwa za uwekezaji na kusisitiza dhamira ya kampuni yake kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuharakisha ajenda ya maendeleo ya viwanda kupitia ubia wa kimkakati.
Aidha, amempongeza Prof. Kitila kwa kuongoza ujumbe wenye nguvu na ulioratibiwa kwa ufanisi, akisema muundo wa ujumbe huo unaonesha dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kutafsiri sera na maono ya uwekezaji kuwa miradi halisi yenye manufaa kwa Taifa.
Amebainisha kuwa uwepo wa viongozi waandamizi na wataalamu kutoka taasisi muhimu unaonesha utayari wa Tanzania kujenga ushirikiano endelevu utakaochochea maendeleo ya viwanda na ukuaji wa uchumi.
Miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa ni mpango wa muda mrefu wa Dangote Group wa kuwekeza hadi dola za Marekani bilioni 46 ifikapo mwaka 2030 katika sekta mbalimbali za kimkakati barani Afrika, ikiwamo Tanzania.
Mazungumzo yalijikita katika kupanua ushirikiano kwenye sekta za viwanda, nishati, madini, uchukuzi, usafirishaji na ugavi (logistics), bandari, miundombinu pamoja na sekta nyingine zenye kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Prof. Kitila alisisitiza dhamira ya Rais Dkt. Samia ya kuendelea kujenga mazingira ya biashara na uwekezaji yaliyo thabiti, shindani na rafiki kwa wawekezaji. Alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi yanayolenga kuboresha miundombinu, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuunda fursa zaidi za ukuaji wa uchumi endelevu, ajira na uhamishaji wa teknolojia.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa Tanzania pia unatarajiwa kutembelea viwanda vya kisasa vya Dangote Group vilivyopo Lagos ili kujionea mifumo ya uzalishaji wa kisasa na usimamizi wa shughuli za ugavi. Ziara hiyo itatoa uzoefu na maarifa yatakayosaidia Tanzania katika azma yake ya kuwa kitovu cha viwanda na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki. Ziara ya Lagos ni hatua nyingine muhimu katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ya Rais Dkt. Samia