Jeshi la Polisi Tanzania limesema hali ya usalama nchini ni shwari na litaendelea kupokea taarifa za nia ya kufanya mikutano ya hadhara pamoja na vikao kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wengine, huku likiwataka waandaaji kuwasilisha taarifa hizo kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) kwa mujibu wa sheria.
Katika taarifa kwa umma aliyoitoa Julai 29, 2026, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, ameeleza kuwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya usalama kurejea kikamilifu kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti mipango ya watu waliokuwa wakihamasisha vitendo vya kihalifu.
DCP Misime amefafanua kuwa katika kipindi cha nyuma, Jeshi la Polisi lilikuwa likiwashauri waandaaji kuahirisha mikutano hiyo kutokana na viashiria vya kiusalama vilivyokuwepo wakati huo.
Msemaji huyo wa Polisi amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliouonesha kwa kuzingatia maelekezo ya vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na kukataa kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu vilivyokuwa vikipangwa na kuhamasishwa na baadhi ya watu.
“Watu hao walikuwa wakielekezana mbinu mbalimbali za kufanikisha malengo yao, ikiwa ni pamoja na kupanga kuua watu, kuchoma moto shule ili kuleta hofu na taharuki kwa wazazi na walezi, kulipua miundombinu ya umeme ya TANESCO, kufunga barabara, pamoja na kuwapora askari silaha. Kitendo cha wananchi kuvikataa vitendo hivyo ndicho kilichochangia nchi kuendelea kuwa shwari,” amesema DCP Misime.
Aidha, DCP Misime amewasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya uhalifu au kubaini watu wanaohamasisha uvunjifu wa amani ili hatua za haraka za kisheria zichukuliwe, akisisitiza kuwa amani na usalama ndio msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.