Latest Posts

RIPOTI YA UCHUMI DUNIANI, YAONESHA MATOKEO MAKUBWA UCHUMI WA TANZANIA CHINI YA RAIS SAMIA

Shirika la Fitch Ratings limethibitisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na alama ya ‘B+’ kwa kuwa na uchumi unaokua kwa kasi na uwezo wa Kulipa Madeni ya Nje kwa Muda Mrefu (IDR) huku ikiendelea kukabili changamoto za kiutawala na mapato.

Taarifa iliyotolewa tarehe 13 Desemba 2024 na shirika hilo inaonesha mwelekeo chanya wa uchumi wa Tanzania huku ikibainisha changamoto za usimamizi wa mapato na mfumo wa sera za uchumi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Pato la Taifa (GDP) la Tanzania linatarajiwa kuongezeka kwa 5.4% mwaka 2024 na kufikia 5.9% mwaka 2025. Hii ni juu ya wastani wa kundi la nchi zilizo katika alama ya ‘B’ ambalo ni 4.7%.

“Ukuaji huu umechangiwa na maendeleo katika sekta za kilimo, utalii, madini, na uwekezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu kama Reli ya Standard Gauge na Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere”, ameeleza Gaimin Nonyane, mchanganuzi wa ripoti hiyo.

Aidha ripoti hiyo imeeleza kuwa mfumuko wa bei nchini umesalia chini ya lengo la 5% lililowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, huku ukiwa wastani wa 3.1% katika robo ya tatu ya 2024. Hii ni kutokana na sera madhubuti za fedha, bei za chini za nishati, na hali nzuri ya hewa iliyoimarisha uzalishaji wa chakula.

Aidha wachanganuzi wa ripoti hiyo wameeleza kuwa akiba ya fedha za kigeni imeimarika, ikitarajiwa kufikia Dola bilioni 5.6 mwishoni mwa mwaka 2024. Hii imetokana na ongezeko la mapato ya utalii na mauzo ya nje, pamoja na kubadilika kwa uratibu wa kiwango cha kubadilisha fedha.

“Akiba ya fedha za kigeni imeimarika, ikitarajiwa kufikia Dola bilioni 5.6 mwishoni mwa 2024, kutoka Dola bilioni 5.4 mwishoni mwa Oktoba. Deni la serikali linabakia wastani, likiwa 48.5% ya GDP mwaka wa fedha 2024, chini kidogo ya wastani wa kundi la ‘B’”, ameeleza Thomas Garreau, Mkurugenzi Mwenza na mchambuzi wa Fitch Ratings.

Kwa upande mwingine, changamoto kadhaa bado zinaendelea kuathiri uwezo wa Tanzania kushindana kimataifa. Fitch imeangazia masuala kama vile udhaifu wa mfumo wa sera za uchumi, utekelezaji dhaifu wa mapato ya serikali, na shinikizo za fedha za kigeni katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024.

Fitch imeeleza kuwa, ingawa kuna juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa kodi, mapato yasiyo ya kodi yamesalia chini ya matarajio kwa 17% katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025. Mapato ya serikali ya kati yanatarajiwa kuongezeka hadi 15.7% ya GDP mwaka wa fedha 2025, lakini bado yapo chini ya wastani wa kundi la ‘B’ wa karibu 18%.

“Ukusanyaji wa mapato unaathiriwa zaidi na changamoto za utekelezaji na udhaifu katika udhibiti wa matumizi. Hali hii inaendelea kuwa kikwazo kwa juhudi za kupunguza nakisi ya bajeti,” ilieleza ripoti ya Fitch.

Fitch imebainisha kuwa mfumo wa sera za uchumi wa Tanzania, pamoja na uwezo wa taasisi, unahitaji maboresho zaidi. Ingawa Benki Kuu ya Tanzania (Bot) imeanza kubadilisha mfumo wake wa sera za fedha kuelekea kwenye mfumo unaozingatia viwango vya riba, changamoto za muda mfupi kama upungufu wa ukwasi zimeathiri ufanisi wa utekelezaji.

“Benki Kuu ya Tanzania imeonesha nia ya dhati katika kuboresha uwezo wa udhibiti wa fedha, lakini changamoto za muundo bado zipo, hususan shinikizo za fedha za kigeni,” imesema Fitch.

Ripoti hiyo imeendelea kueleza kuwa Tanzania inaendelea kunufaika na uwekezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu. Miradi kama Reli ya Standard Gauge na Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere inaongeza ajira, usafirishaji, na upatikanaji wa nishati. Sekta za utalii na madini pia zimeimarika, huku maendeleo ya muda mrefu yakitegemewa kutoka kwenye uchimbaji wa gesi asilia na uzalishaji wa LNG.

Alama ya ‘B+’ ya Tanzania inaonesha kwamba, licha ya changamoto zinazokumba uchumi, kuna mwelekeo mzuri wa ukuaji wa muda mrefu. Baadhi ya wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa mwelekeo huu unatokana na sera zilizowekwa na Serikali ya Rais Samia katika kuweka kipaumbele nidhamu ya kifedha, ikihakikisha kuwa deni la serikali linabakia katika kiwango cha wastani cha asilimia 48.5 ya GDP katika mwaka wa fedha wa 2024.

Aidha imeelezwa kuwa mkazo wake katika mikopo yenye masharti nafuu na matumizi bora ya rasilimali umehakikisha deni linabakia kuwa la kudumu huku rasilimali zikitumika katika miradi yenye manufaa makubwa. Licha ya maendeleo hayo, serikali na wadau wa uchumi wanapaswa kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto za mapato na sera za uchumi ili kuhakikisha uthabiti wa kifedha na mafanikio ya kiuchumi kwa kizazi kijacho.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!