Katika mkutano wa kilele wa Financial Times Africa uliofanyika London hivi karibuni Mwenyekiti wa Taifa Group Ltd., Rostam Aziz, amezungumzia umuhimu wa mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na kampuni ya DP World katika kuboresha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Rostam amesisitiza umuhimu wa mkataba huo kwa kuzingatia kuwa Tanzania iko katika eneo muhimu kijiografia na kuzungukwa na nchi saba zinazoitegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya biashara.
“Tanzania iko katika eneo nzuri kijiografia. Ina nchi saba zinazozunguka, na nchi zote hizi zinategemea Bandari ya Dar es Salaam,” amesema Rostam, akiongeza kuwa, “Uzoefu wetu na uendeshaji wa bandari kabla ya hili umekuwa wa kusikitisha, na ufanisi umekuwa wa kiwango cha chini sana. Tumekuwa na meli zinazongoja kwa muda mrefu bandarini, jambo ambalo linagharimu sana watumiaji wa mwisho na uchumi kwa ujumla.”
Kwa mujibu wa Rostam, uzoefu wenye upungufu wa uendeshaji wa bandari uliwahi kutokea pia wakati Tanzania ilipokuwa na ushirikiano na kampuni ya Hutchison kutoka Hong Kong, ambapo alisema kutokana na umbali na tofauti ya wakati, ufanisi haukuwa mzuri. Amefafanua kuwa DP World ni mshirika anayefaa kwa sababu ya rekodi nzuri na maslahi ya kijiografia yenye kuzingatia mahitaji ya Dar es Salaam, akisema kuwa uwekezaji huo ni njia ya kuhakikisha ufanisi na kuimarisha uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
“Ikiwa utaenda Dar es Salaam na kutazama baharini, utaona kama vile kuna miti mingi ya Krismasi kutokana na meli nyingi zinazongoja kutia nanga. Hivyo basi, tulihitaji kutafuta mwendeshaji mwenye uzoefu, rekodi nzuri, na maslahi kijiografia kuhusu Dar es Salaam, na tulipofanya tathmini tuliona kwamba DP World ndiyo mshirika bora zaidi tunaweza kuwa naye”, ameeleza Rostam.
Aidha amezungumzia kuhusu Mradi wa Gesi Asilia (LNG), Rostam ameeleza kuwa mradi huu ulikuwa unastahili kuanzishwa mwaka 2014, lakini kutokana na changamoto mbalimbali, haukuweza kufikia hatua hiyo. Ameeleza matumaini yake kuwa mradi huo utaleta mabadiliko makubwa kwa uchumi wa Tanzania.
Rostam ametoa mfano wa makubaliano ya mafanikio yaliyofikiwa na kampuni ya Barrick Gold, ambapo Tanzania na Barrick hufaidika kwa mgawanyo wa faida ya asilimia 50 kwa 50. Amependekeza kuwa, kama ambavyo sekta ya madini imefanikiwa, sekta ya gesi asilia inapaswa kufuata nyayo hizo ili kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na rasilimali zao za asili.
“Mwaka jana, Barrick ilikuwa mlipaji mkubwa wa kodi nchini Tanzania na pia mchangiaji mkubwa wa gawio kwa serikali ya Tanzania. Kwa hivyo tungependa kuona kwamba kile tulichofanya kwenye sekta ya madini kinaweza pia kufanywa kwenye sekta ya gesi asilia (LNG) ili uchumi na wananchi wanufaike na rasilimali hizi za asili.”, ameeleza Rostam.
Rostam pia ametumia jukwaa hilo kuzungumzia changamoto zinazokabili nchi za Afrika katika kupata mikopo yenye riba nafuu. Ametoa wito kwa mashirika ya kimataifa na makampuni ya fedha kuacha ubaguzi wa kijiografia dhidi ya Afrika na kuweka viwango vya riba sawa na maeneo mengine duniani.
“Kwa mfano, Ufilipino au Iraq hupata kiwango cha riba cha chini ikilinganishwa na Botswana, ambayo ni uchumi wa kiwango cha uwekezaji. Kwa hiyo, kuna upotoshaji wa viwango na bei kwa Afrika. Tunahitaji hatua za haraka kuchukuliwa”, ameeleza.
Aidha, Rostam ametoa wito kwa nchi zilizoendelea za G7 na mashirika ya kibenki kuweka sera ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa Afrika.
“Kwa mujibu wa ripoti ya Moody mwaka 2021 iliyohusu kampuni 800 kote duniani, kiwango cha kushindwa kulipa madeni Afrika kilikuwa chini ya 2%, Ulaya ilikuwa takriban 5%, Amerika Kusini ilikuwa takriban 12%, na Marekani ilikuwa takriban 6%. Kwa hiyo, unaweza kuona kwamba Afrika ina uwezekano mdogo wa kushindwa kulipa madeni, lakini bado tunaadhibiwa.”
Mkutano wa Kilele wa Financial Times Africa ulihudhuriwa na wakuu wa nchi, Magavana wa Mabenki Kuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Mawaziri wa Uingereza, IMF, Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa, mabenki, na wadau wengine.