Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, amesema kuwa ndani ya siku 60 wizara yake itakuwa imepata ufumbuzi wa malalamiko ya wawekezaji kuhusu tozo ya shilingi 150,000 inayotozwa kwa kushusha na kupakia makontena kwenye halmashauri mbalimbali.
Kauli hiyo ameitoa siku ya Jumatatu Februari 10, 2025 baada ya mkutano wake na wanachama wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), ambao wameeleza kuwa tozo hiyo inaongeza gharama za uzalishaji na kuathiri ushindani wa viwanda katika soko.
Waziri Jafo amesema kuwa Serikali imepokea malalamiko hayo na tayari imeanza mchakato wa kutafuta suluhisho kwa kushirikiana na wadau husika.



“Changamoto hii inahusisha sekta mbalimbali, hivyo tunaratibu kikao cha pamoja na wizara na mamlaka husika ili kupata suluhisho la kudumu. Tumekubaliana kwamba ndani ya siku 60 tutakuwa tumepata majibu,” amesema Waziri Jafo.
Amesisitiza kuwa malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha viwanda vinaendelea kukua na uwekezaji unaimarika kwa ajili ya kuongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa taifa.
“Sekta binafsi ndiyo mwajiri mkuu duniani, hivyo Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ili kuhamasisha ajira na ujasiriamali kwa vijana wetu,” ameongeza.
Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodgar Tenga, alisema shirikisho hilo limefarijika kuona Serikali ikijitokeza kuwasikiliza wafanyabiashara.
“Tozo hii inaongeza gharama za uzalishaji na kufanya bidhaa zetu kushindwa kushindana kwenye soko. Tunamshukuru Waziri kwa kusikiliza hoja yetu, na tunaamini ndani ya siku 60 tutapata suluhisho,” amesema Tenga.



Ameongeza kuwa maendeleo ya viwanda yanategemea mazingira rafiki ya biashara, na hivyo Serikali inapaswa kuhakikisha tozo zisizo na tija zinapunguzwa au kuondolewa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila, amesema kuwa tozo hizo hazitozwi kiholela, bali ni halali kwa mujibu wa sheria ndogo za Manispaa za Temeke, Kinondoni, Ilala, Ubungo na Kigamboni.
“Mkoa umeshakaa vikao viwili na CTI kujadili changamoto hii, na baadhi ya hoja zimeshapatiwa ufumbuzi huku nyingine zikiendelea kushughulikiwa,” alisema Dk. Nguvila.
Ameongeza kuwa Serikali haitaki kuona changamoto zinazokwamisha sekta ya viwanda, kwani sera ya Rais Samia ni kukuza maendeleo ya viwanda kwa kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki kwa wawekezaji wote.