Latest Posts

SHABAHA ZA JUMLA ZA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050

Jumatano tarehe 11 Desemba 2024 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amezindua Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, katika hafla iliyofanyika Visiwani Zanzibar.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050) inalenga kuwa na taifa jumuishi, lenye ustawi, haki, na linalojitegemea kuelekea mwaka 2050. Katika kufikia njozi hii, Rasimu ya Dira 2050 imependekeza shabaha zifuatazo:

  1. Tanzania kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati ngazi ya juu, ikichagizwa na sekta ya uzalishaji viwandani. Lengo ni kufikia pato la mtu, kati ya Dola za Marekani 4,700 na 8,000, na pato la taifa kufikia zaidi ya bilioni 700 za Dola za Marekani ifikapo mwaka 2050.
  2. Kuondoa umaskini uliokithiri na kupunguza kiwango cha umaskini wa mahitaji kuwa chini ya asilimia 5.
  3. Tanzania kuwa nchi kinara katika uzalishaji wa chakula barani Afrika, na kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa kumi wa chakula duniani.
  4. Kuwa na mazingira bora ya kufanya biashara, na kushika nafasi ya tatu bora barani Afrika katika kuvutia wawekezaji.
  5. Kuwa na sekta binafsi imara na yenye ujasiri na uwezo wa kushindani kikanda na kimataifa.
  6. Kiswahili kuwa lugha inayoheshimika na kutumika kama moja ya lugha mbili rasmi katika ukanda wa Afrika na moja ya lugha rasmi zinazotumika katika Jumuiya ya Umoja wa Mataifa.
  7. Kuwa na mfumo bora wa elimu katika ngazi zote unaojenga maarifa na stadi za wahitimu na wenye kushabihiana kwa karibu na sekta za uzalishaji.
  8. Kuwa na jamii yenye afya njema ambapo kila mtanzania anapata huduma bora za afya, maji na hifadhi ya jamii.
  9. Kuwa taifa linalojitegemea katika mahitaji ya umeme ambapo wastani wa matumizi ya umeme kwa mtu yatakuwa angalau kWh 600.
  10. Kuwa na jamii inayothamini uhifadhi wa mazingira na iliyo tayari kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
  11. Tanzania kuwa kitovu cha huduma za usafirishaji mizigo ya kibiashara katika ukanda wa Afrika.
  12. Kuwa na jamii yenye maarifa ya kidijiti na yenye uwezo wa kutumia zana na kuzalisha teknolojia za kidigiti katika huduma na uzalishaji.
  13. Tanzania kuwa taifa la kidemokrasia, likiongozwa na katiba imara inayoakisi mwafaka wa kitaifa, taasisi madhubuti za umma, na mfumo thabiti wa vyama vingi vya siasa.
  14. Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 bora duniani na kushika nafasi ya kwanza barani Afrika katika kupunguza pengo la kijinsia kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2050.
  15. Kuongeza wastani wa umri wa kuishi kwa wanaume na wanawake kufikia miaka 75.
  16. Tanzania kuwa nchi kinara barani Afrika kwa vivutio vya utalii na miongoni mwa nchi tatu bora barani Afrika zinazotembelewa na watalii kwa wingi.
  17. Kila Mtanzania kuwa na elimu angalau ya kidato cha nne, na angalau asilimia 15 ya Watanzania kuwa na elimu ya juu, wakiwa na ujuzi stahiki unaolingana na mahitaji ya soko la ajira na ulimwengu unaobadilika.
  18. Angalau mtu mmoja katika kila watanzania wawili wenye sifa za kuajiriwa kuwa wameajiriwa katika sekta rasmi na wakiwa na mikataba kamili ya ajira.
  19. Watanzania wote wanafurahia uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kukusanyika katika mazingira ya amani, usalama na utulivu.
  20. Ardhi yote ya Tanzania kupangwa na kupimwa kwa matumizi mbalimbali, ikiwemo ardhi kwa ajili ya makazi bora, kilimo, mifugo na uwekezaji.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!