Latest Posts

SHIRI UNITED SPORTS ACADEMY YAWAPA NAFASI WATOTO KUFANIKISHA NDOTO ZA SOKA

Shiri United Sports Academy, iliyopo wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, imeanza mchakato wa kuwabaini watoto wenye vipaji vya soka kupitia shindano maalum lililopewa jina “Nyota Challenge”. Lengo ni kuwajengea uwezo watoto hao ili waweze kutimiza ndoto zao za kucheza mpira wa miguu katika viwango vya kimataifa.

Mwenyekiti wa Shiri United Sports Academy, Robert Msemo, amesema kuwa shindano hilo lina lengo la kupata wachezaji wenye uwezo wa kucheza soka la kimataifa na kuwapatia fursa za masoko ndani na nje ya nchi.

“Tumeweza kupata watoto 167 kutoka shule kumi za msingi katika Kata ya Mnadani. Awali, tulilenga kuchukua watoto 60 tu, lakini kutokana na vipaji vilivyooneshwa, tumeamua kuwachukua wote. Watakuwa kwenye mazoezi kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita,” amesema Msemo.

Kwa upande wake, Afisa Utamaduni na Michezo wa Wilaya ya Hai, Faston Kagimbo, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amepongeza jitihada za Shiri United Sports Academy na kuahidi kuendelea kushirikiana nao kuhakikisha watoto hao wanapata mazingira mazuri ya kufanikisha ndoto zao.

“Miundombinu ya michezo wilayani Hai inaboreshwa, hasa viwanja vya shule na vile vya kijamii, ili kutengeneza mazingira mazuri ya michezo,” amesema Kagimbo.

Kassim Shaki, Afisa wa Azania Benki, tawi la Moshi, ambayo ndiyo mdhamini wa shindano hilo, amesema michezo si burudani pekee bali ni fursa muhimu ya ajira, biashara, na mafanikio.

“Azania Benki tupo kwa ajili ya kukuza vipaji na kuwanyanyua kupitia fursa mbalimbali. Shindano la Nyota Challenge tutalitizama kwa karibu ili mafanikio yaonekane. Tumekuwa tukishiriki pia katika ligi ya mkoa wa Kilimanjaro na kufanikisha mengi,” amesema Shaki.

Shindano hili linaonesha matumaini makubwa kwa watoto wenye vipaji, huku likiwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao na kujijengea mustakabali wa baadaye katika ulimwengu wa soka.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!