Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steven Mengele maarufu kwa jina la Steve Nyerere, amempongeza Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kwa kile alichokiita “ukomavu wa kisiasa, uzalendo na uthubutu wa kuonesha mshikamano wa kitaifa” baada ya Mbowe kushiriki hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 jijini Dodoma.
Katika hafla hiyo ya kitaifa, iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, vyama vya siasa, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, Mbowe alionekana akisalimiana na viongozi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, huku akishiriki picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa nchi.
Akitoa maoni yake kupitia mitandao ya kijamii, Steven Mengele amesema kuwa kitendo cha Mbowe kuhudhuria tukio hilo muhimu kwa mustakabali wa taifa ni mfano wa kuigwa kwa wanasiasa wa sasa na hasa vijana wanaojitokeza katika medani ya siasa.
“Mbowe ameonyesha ukomavu mkubwa sana. Umeonyesha uzalendo kwa Taifa lako. Hukuangalia lolote mbele yako zaidi ya kuhakikisha Taifa linasonga mbele. Maendeleo hayana itikadi – ni faida kwa kila Mtanzania,” amesema Mengele.
Akiendelea kusisitiza umuhimu wa siasa za mshikamano na maelewano, amesema vijana wengi wamekuwa wakidhania siasa ni kugombana, kupinga au kukosoa kila jambo, hali ambayo alisema inapaswa kubadilishwa kwa kujifunza kupitia mifano kama ya Mbowe.
“Mheshimiwa Mbowe wewe ni mfano wa kuigwa. Kuna la kujifunza kupitia wewe – hasa kwa vijana wanaodhani siasa ni kupinga tu, kutukana na kukosoa. Wanasahau kuwa siasa ni umoja wa kweli kwenye kuhakikisha taifa linasonga mbele,” ameongeza.
Mengele amesisitiza kuwa, licha ya Mbowe kuwa Mwenyekiti Mstaafu wa CHADEMA, ana haki ya kushiriki mijadala na shughuli yoyote yenye maslahi kwa taifa, huku akionya dhidi ya viongozi wa kisiasa na wanaharakati “uchwara” wanaobeza ushiriki wake katika tukio hilo.
“Wanasiasa uchwara na wanaharakati uchwara wanashindwa kutofautisha kuwa wewe ni Mwenyekiti mstaafu. Una haki ya kushiriki kwenye kila jambo lenye tija kwa taifa. Umeamua kunyamaza kuhusu migogoro ya chama chako – hiyo ni hekima. Lakini umetoa macho yako kwa utaifa, maendeleo na amani ya Tanzania,” amesema.
Katika hitimisho la ujumbe wake, Mengele amesema Mbowe ameonesha kuwa siasa si uadui bali ni jukwaa la kuchochea maendeleo na mshikamano, na kwamba hatua yake imefungua milango ya fikra mpya miongoni mwa wanasiasa wa kizazi kipya.