Benki ya NMB imekabidhi vifaa vya kujifungulia kwa wajawazito 300 pamoja na mashuka 300 kwa Hospitali ya Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya tamasha la kumbukumbu ya Bibi Titi Mohamed. Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 12.3 vilikabidhiwa na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Seka Urio, katika hafla iliyofanyika Utete, Rufiji.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Seka amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada za NMB za kurudisha fadhila kwa jamii kupitia miradi ya maendeleo katika sekta za afya na elimu. “Vifaa hivi ni sehemu ya uwajibikaji wa benki yetu kwa jamii, ambapo tumekuwa tukitenga asilimia 1 ya faida yetu kila mwaka kwa ajili ya kusaidia miradi ya kijamii,” amesema.
Aidha, Seka amebainisha kuwa NMB imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma za kijamii kwa zaidi ya muongo mmoja, hususan katika nyakati za majanga, na kwamba benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali kutatua changamoto mbalimbali nchini.
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, aliyepokea msaada huo kwa niaba ya serikali, ameishukuru NMB kwa mchango wake muhimu katika kuboresha huduma za afya Rufiji. Amesema msaada huo si tu unawasaidia wajawazito, bali pia unamuenzi mpigania uhuru na Mbunge wa kwanza wa Rufiji, Bibi Titi Mohamed.
“Mmemuenzi Bibi Titi Mohamed, ambaye alikuwa mama wa kwanza kupigania uhuru wa taifa letu. Huu ni mfano mzuri wa uzalendo na ushirikiano katika maendeleo ya jamii,” amesema Mchengerwa.
Pia, Waziri huyo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuwasaidia wanawake na kuimarisha huduma za afya nchini. “Rais wetu ni mama anayejali wanawake na wananchi wote. Juhudi za benki ya NMB ni sehemu ya maono yake ya kuboresha maisha ya Watanzania,” ameongeza.
Msaada huo umetajwa kuwa ni mkombozi kwa akinamama wa Rufiji, huku ukionesha mshikamano wa sekta binafsi na serikali katika kuboresha huduma za kijamii na kuinua hali ya maisha ya Watanzania.