Na Theophilida Felician.
Katibu mkuu wa chama cha waganga wa tiba asili nchini TAMESOT Bw Lukas Joseph Mlipu kwa niaba ya wanachama wenzake ameelezea namna walivyopokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha spika mstaafu Job Yustino Ndugai kilichotokea Tarehe 6 Agost 2025 jijini Dodoma.
Katibu huyo akizungumza na chombo hiki kwa njia ya simu akiwa katika mwendelezo wa ziara ya kuhamasisha waganga kushiriki wiki ya tiba asili ya mwafrika Mbarali mkoani Mbeya amesema Marehemu Job Ndugai alikuwa ni mchango mkubwa kwa chama kwani alitoa ushauri wa karibu na wenye kukijenga, aliwahi kuwa msaada kwa chama baada ya kukisaidia mawazo yenye kuutatua mgogoro uliokuwa ndani ya chama mwaka 2018 na kutatuliwa 2019 kipindi hicho akiwa spika wa Bunge.
Amesema kutoka na ushauri wake chama kilisimama imara na sasa kinaendelea vizuri, hivyo hadi umauti unamkuta alikuwa ameishatoa ahadi ya kuunga mkono chama kwa kutoa mchango juu ya kusaidia ujenzi wa ofisi ya chama taifa iliyojengwa mamlaka ya mji mdogo Kibaigwa Dodoma.
“Ni mambo mengi tumeshirikiana naye hata baada ya kustaafu uspika hususani alipokuwa akishiriki matukio ya kijamii TAMESOT tulihakikisha tunaungana naye bega kwa bega, hakika tutaendelea kumkumbuka daima aliitambua na kuithamini tiba asili kwa nguvu zote tumempoteza mtu muhimu sana” Katibu Mkuu Lukas Joseph Mlipu.

Kufuatia kifo hicho ametoa pole kwa familia, wananchi wa Kongwa na serikali kwa ujumla huku akiwasihi wanachama kuwa watulivu kipindi hiki kigumu na kuendelea kumuombea dua njema na yenye kumtakia mapumziko mema.