Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania- Zanzibar (TAMWA ZNZ) kimeeleza dhamira yake ya kutumia Siku ya Kimataifa ya Redio kama jukwaa la kutathmini mchango wa redio katika maendeleo ya jamii, hususan katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Katika kuadhimisha siku hiyo, TAMWA ZNZ inatarajia kukutana na wadau wa habari mnamo Februari 12, 2025, katika ofisi zake zilizopo Tunguu, Zanzibar. Mkutano huo utawakutanisha wahariri, wakuu wa vipindi, waandishi wa habari, na viongozi wa vyombo vya habari kutoka Unguja na Pemba kwa lengo la kujadili nafasi ya redio katika kuelimisha na kuchochea mijadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa, kaulimbiu ya mwaka huu, “Redio na Mabadiliko ya Tabianchi”, inalenga kuhamasisha vyombo vya habari kutumia redio kama nyenzo ya kuielimisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na njia za kukabiliana nazo.
TAMWA ZNZ inasema kuwa, licha ya umuhimu wa redio katika kufikisha taarifa, tafiti zinaonesha kuwa redio bado haijatumika ipasavyo kuzungumzia masuala ya tabianchi. Utafiti uliofanywa mwaka 2024 na chama hicho umebaini kuwa kati ya vipindi 2,600 vilivyorushwa na ZBC na Assalam Radio, ni vipindi 11 pekee (asilimia 0.9%) vilivyohusu mabadiliko ya tabianchi.
“Tafiti zinaonesha kuwa sauti za wanawake hazipewi nafasi ipasavyo katika mijadala ya tabianchi. Tunaziomba redio na vyombo vingine vya habari kuandika zaidi kuhusu wanawake na nafasi yao katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” anasema Dkt. Mzuri.
Kwa mujibu wa TAMWA ZNZ, redio ina nafasi muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, kuhimiza matumizi ya mbinu endelevu za kilimo, uhifadhi wa mazingira, na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Mbali na suala la tabianchi, TAMWA ZNZ inasisitiza kuwa redio imeendelea kuwa chombo madhubuti cha kupigania haki za wanawake na watoto, usawa wa kijinsia, na ushiriki wa wanawake katika uongozi.
Katika mwaka 2024 pekee, TAMWA ZNZ ilichapisha habari 778 kupitia vyombo mbalimbali vya habari, zikiwemo 101 kwenye redio. Habari hizo zilihusu masuala kama vile udhalilishaji wa kijinsia, afya ya uzazi, wanawake katika uongozi, na uhuru wa habari.
TAMWA ZNZ inatoa shukrani kwa vyombo vya habari kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kwa wakati. Chama hicho kinapongeza juhudi za redio kufikisha ujumbe kwa jamii, hasa katika maeneo ya pembezoni ambapo vyombo vingine vya habari vinafikia kwa ugumu.
Siku ya Kimataifa ya Redio huadhimishwa Februari 13 kila mwaka tangu ilipotangazwa rasmi na UNESCO mwaka 2011 na kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2013. TAMWA ZNZ inazitakia redio zote maadhimisho mema na mafanikio katika mipango yao ya baadaye.