Latest Posts

TANZANIA YAENDELEA KUNG’ARA UIMARA WA KIUCHUMI: RIPOTI YA IMF YATHIBITISHA UDHIBITI IMARA WA DENI LA TAIFA

Ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuhusu hali ya deni duniani imeonyesha kuwa Tanzania inazidi kuimarika kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Katika ripoti ya Economic Outlook ya Oktoba 2024, Tanzania imeorodheshwa na uwiano wa deni kwa uchumi wa asilimia 47%, kiwango kinachothibitisha usimamizi bora wa uchumi ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika na duniani. Hali hii inadhihirisha uwezo wa serikali katika kudhibiti mikopo huku ikiendelea kuwekeza katika miradi yenye tija kwa taifa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wastani wa deni kwa uchumi wa mataifa ya Afrika ni asilimia 67%, jambo linaloonyesha kuwa Tanzania imefanikiwa kusimamia fedha zake vizuri zaidi ikilinganishwa na nchi nyingi za bara hili. Takwimu zinaonesha hali ya deni kwa majirani wa Tanzania, ambapo Kenya ina asilimia 70%, Rwanda asilimia 71%, Uganda asilimia 51%, Malawi asilimia 84%, Msumbiji asilimia 96%, Namibia asilimia 67%, na Ghana asilimia 82%. Takwimu hizi zinaweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi ya kiuchumi, hasa ukizingatia mazingira magumu ya kiuchumi yanayozikabili nchi nyingi za Afrika.

Tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka 2021, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha usimamizi madhubuti wa uchumi kupitia sera thabiti zinazolenga kuimarisha matumizi ya fedha za umma. Miradi mikubwa kama reli ya kisasa ya SGR, bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, na maboresho ya bandari yamefadhiliwa kwa namna inayohakikisha deni la taifa halifiki katika viwango vya hatari.

Mbali na hilo, serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji nchini, hatua ambayo imeongeza mapato ya ndani, kupunguza utegemezi wa mikopo, na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya kimataifa. Mafanikio haya yanatokana na usimamizi thabiti wa fedha za umma, mazingira bora ya uwekezaji, na uwekezaji katika miradi ya maendeleo yenye tija badala ya matumizi yasiyo na maana. Serikali imeonyesha dira thabiti ya kuhakikisha kila shilingi inayotumika inaleta manufaa kwa wananchi.

Ripoti ya IMF ni ushahidi wa wazi kuwa Tanzania imefanikiwa kudhibiti deni lake huku ikiendelea kufanikisha maendeleo ya kiuchumi. Rais Samia ameonyesha weledi mkubwa katika usimamizi wa uchumi, jambo linalofanya juhudi za serikali kutambuliwa kimataifa. Wakati baadhi ya watu wakikosoa sera za serikali, ripoti hii inatoa picha tofauti na kuonyesha umuhimu wa kuunga mkono juhudi za serikali badala ya kukosoa bila kutoa suluhisho. Tanzania iko kwenye mkondo sahihi wa maendeleo, huku ikionyesha mfano wa uongozi bora unaojali maslahi ya taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!