
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wameendelea kupanua wigo wa utekelezaji wa miradi ya kuboresha mazingira ya kujifunzia katika shule mbalimbali nchini. Kupitia ushirikiano huo, kiasi cha takribani shilingi bilioni 1.4 kimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa, hatua inayolenga kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira salama, rafiki na yenye kuchochea ujifunzaji.
Katika kikao kilichofanyika Novemba 19, 2025 katika Makao Makuu ya TEA jijini Dodoma, pande zote mbili zilijadili maendeleo na mpango wa utekelezaji wa mradi huo. Wawakilishi wa UNICEF wakiongozwa na Mtaalamu wa Elimu, Dkt. Ayoub Kafyulilo, walitoa shukrani kwa TEA kwa usimamizi thabiti na ushirikiano mzuri unaowezesha miradi kukamilika kwa wakati. Dkt. Ayoub alisisitiza kuwa ufanisi huo ndiyo umewezesha kuongeza miradi mipya ya ukarabati wa matundu ya vyoo na madarasa ili kunufaisha shule nyingi zaidi.
Akiutambulisha mradi Dkt. Ayoub amesema, fedha hizo takribani bilioni 1.4 zitatumika kwenye shule zaidi ya 75 katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Songwe. Ukarabati huo unatarajiwa kuongeza ubora wa mazingira ya kujifunzia, kupunguza changamoto za utoro na kuwawezesha wanafunzi kupata fursa sawa za elimu bila kujali hali ya mazingira wanayotoka.
Akizungumza kuhusu dhamira ya miradi hiyo, Afisa Elimu kutoka UNICEF, Bi. Sonia Preite, alisema malengo makuu ni kuhakikisha watoto wote wanasoma katika mazingira bora, salama na ya kujenga ari ya ufaulu. Alibainisha kuwa changamoto za miundombinu zimekuwa zikiathiri upatikanaji wa elimu bora, hivyo uwekezaji katika miundombinu ni hatua muhimu katika kuhakikisha usawa na ubora wa elimu kwa kila mtoto.
Kwa upande wa TEA, Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi ya Elimu, Bw. Masozi Nyirenda aliahidi kuwa, TEA itaendelea kushirikiana kwa karibu na UNICEF ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati. Alisisitiza kuwa TEA imedhamiria kuendeleza ubora na usimamizi wa miradi ili kuleta matokeo chanya kwa jamii na sekta ya elimu kwa ujumla.
Awali, TEA na UNICEF walitia saini makubaliano maalumu ya kutekeleza miradi ya ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya elimu katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Songwe. Kupitia makubaliano hayo, kiasi cha takribani shilingi bilioni 2.5 kimetumika kutekeleza miradi 48 hadi kufikia sasa, hatua inayoonesha dhamira ya dhati ya kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia hapa nchin