Latest Posts

TGNP YATINGWA NA MZOZO WA UONGOZI, WANACHAMA WAJA JUU, WADAI KATIBA IFUATWE KATIKA UTEUZI WA UONGOZI

Migogoro ya uongozi ndani ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) imeibua maswali makubwa kuhusu uwajibikaji wa Bodi ya Wakurugenzi, Sekretarieti ya TGNP, na mamlaka ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs).

Wanachama wa TGNP wameeleza masikitiko yao kupitia waraka uliotolewa rasmi siku ya Jumatano tarehe 9 Januari 2025, wakilalamikia ukiukwaji wa Katiba ya TGNP na hatua za Msajili ambazo wanadai zinakiuka uhuru wa taasisi hiyo kujiendesha.

Waraka huo, uliotolewa na zaidi ya 50% ya wanachama wa TGNP, umedai kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo imekiuka maamuzi ya Mkutano Mkuu wa wanachama kuhusu uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji mpya.

Kwa mujibu wa waraka huo, mchakato wa kumteua Mkurugenzi Mtendaji (MM) mpya ulianza mwaka 2021 lakini umekumbwa na ukiukwaji wa taratibu za kikatiba. Kamati ya Ajira ilikamilisha kazi yake na kuwasilisha mapendekezo kwa Bodi mnamo Oktoba 2024. Hata hivyo, Bodi ilikataa mapendekezo hayo na kumuongezea muda Mkurugenzi aliyepo ambaye ni Lilian Liundi, licha ya mkataba wake kufikia ukomo Novemba 2024.

“Ni muhimu kufuata Katiba katika uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji. Mamlaka ya ajira yapo mikononi mwa Mkutano Mkuu, ambao tayari ulitekeleza wajibu wake kwa kumpata Mkurugenzi mpya,” wanachama wamesema katika taarifa yao.

Wanachama wanalalamika kuwa Mkutano Mkuu wa dharura uliopangwa kujadili suala hilo ulizuiliwa na Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Lorenz Vickness Mayao kwa maelekezo ya simu. Baadaye, Msajili alitoa barua rasmi kuzuia mkutano huo, akidai kuwepo kwa “mgogoro” ndani ya shirika.

Wanachama wa TGNP wameeleza kutoridhishwa na hatua za Msajili kuunda Kamati ya kusimamia mifumo ya shirika na kuzuia mabadiliko yoyote ya uongozi hadi ripoti ya kamati hiyo itakapokamilika.

“Msajili amekuwa akichukua hatua zinazovuka mamlaka yake kisheria, ikiwa ni pamoja na kusikiliza upande mmoja wa madai ya mgogoro ambao haujawasilishwa kwa vyombo halali vya shirika,” waraka unasema.

Barua ya Msajili ya tarehe 3 Desemba 2024 ambayo Jambo TV tumepata kuiona inaeleza kuwa Kamati hiyo inatakiwa kujenga uwezo wa viongozi wa TGNP, kusimamia chaguzi za ndani, na kuimarisha mifumo ya kitaasisi ndani ya siku 60. Hata hivyo, wanachama wanasema hatua hiyo ni kuingilia uhuru wa shirika na kupuuza Katiba ya TGNP.

Waraka huo umeibua maswali kadhaa ikiwamo kutaka kufahamu sababu ya Msajili kuingilia mchakato wa ndani wa TGNP katika kile kilichoelezwa ‘bila kufuata utaratibu wa Katiba?”, Ni nani aliwasilisha madai ya mgogoro kwa Msajili na kwa maslahi gani na kwa nini Bodi imekuwa ikipinga ukaguzi wa kiuhasibu kwa zaidi ya miaka mitatu?

Pengine walau Jambo TV tungeweza kupata majibu ya maswali haya, lakini tulipomtafuta Mkurugenzi Mkuu wa TGNP siku za nyuma alielekeza jambo hili atafutwe Mwenyekiti wa Bodi, Gemma Sware Akilimali kulizungumzia ambaye naye tulimtafuta, hata hivyo alisisitiza suala hilo ni la ndani ya TGNP na kama kuna vyanzo vinatupa taarifa juu ya jambo hilo tuendelee kutafuta taarifa kutoka kwa vyanzo hivyo pekee.

Wanachama wanasema hatua za Msajili na Bodi zimeathiri uendeshaji wa shirika hilo na kuondoa imani ya umma katika utendaji wake.

Wanachama wa TGNP wamesisitiza kuwa mabadiliko ya uongozi lazima yafanyike kwa kuzingatia Katiba ya shirika. Wametaka uwajibikaji wa Bodi na Sekretarieti, pamoja na hatua za kurejesha imani ya umma kwa TGNP.

“Ni muhimu kwa vyama visivyo vya kiserikali kuruhusiwa kujiendesha kwa mujibu wa Katiba na bila kuingiliwa na mamlaka za nje,” wanachama wamesema.

Wanachama wa TGNP wamesisitiza kuwa mustakabali wa shirika hilo unategemea uongozi wa kikatiba na uwazi wa maamuzi. Wameahidi kuendelea kupigania haki na uwajibikaji ndani ya shirika hilo kwa maslahi ya wanachama na jamii kwa ujumla.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!