Latest Posts

TIC YAONGOZA KAMPUNI 60 KUTOKA JAPAN KUTEMBELEA KONGANI YA VIWANDA BAGAMOYO, PIA YAELEZA UNAFUU ULIOPO KWA WATANZANIA KUWEKEZA

 

Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, amesema kuwa hatua ya kimapinduzi iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuzindua Kamati ya Kitaifa ya Kufanya Mapitio na Maboresho ya Mifumo ya Kodi, itasaidia sana kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

“Kwa takribani mwaka na nusu, TIC imekuwa ikifuatilia changamoto zinazowakumba wawekezaji na wafanyabiashara, eneo lililopigiwa kelele sana ni katika eneo la kodi. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maamuzi ya kuunda timu ya kupitia Mapitio na Maboresho ya Mifumo ya Kodi hiyo ni baada ya kupokea maoni katika Baraza la Taifa la Biashara lililofanyika mwezi Julai mwaka huu.” alisema Teri

Mkurugenzi Teri alieleza kuwa timu hiyo, itakapokamilisha kazi yake na kutoa mapendekezo kwa Rais, itasaidia kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.

Ameongeza kuwa Rais Samia ni kiongozi msikivu ambaye anathamini uwekezaji kama nyenzo muhimu ya kuwatoa Watanzania kwenye umasikini.

Amesisitiza kuwa, kwa maboresho hayo, Tanzania itakuwa nchi bora zaidi kwa uwekezaji barani Afrika, kwani maeneo mengine kama sheria, uhuru wa mahakama, na ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali tayari yameboreshwa.

“Eneo pekee linalohitaji kuboreshwa zaidi ni mfumo wa kodi, na kwa jitihada za Rais Samia, linaenda kuimarishwa kwa kiasi kikubwa.”

Teri amesema hayo Oktoba 05, 2024 akiongoza ujumbe wa kampuni 60 kutoka Japan pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Japan Mheshimiwa Baraza Luvanda kutembelea kongani ya Viwanda Bagamoyo mkoani Pwani.

Ameongeza kwa kusema kuwa, TIC pia imeimarisha huduma zake kwa wawekezaji, ikiwemo kuharakisha upatikanaji wa vibali. Maboresho hayo yanalenga kuhakikisha kwamba uwekezaji unaendelea kukua, ajira zinapatikana, serikali inapata mapato, na teknolojia mpya zinaingia nchini, jambo ambalo litasaidia sana kukuza uchumi wa Tanzania.

Kuhusu ukuaji wa sekta mbalimbali, Mkurugenzi Teri ametaja kuwa sekta inayoongoza kwa ukuaji ni viwanda, ikifuatiwa na ujenzi, uchukuzi, uhifadhi wa bidhaa za kilimo na viwandani, pamoja na utalii na kilimo.

Kati ya Januari na Machi mwaka huu, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 109 ya viwanda, na hivyo kwa wastani imekuwa ikisaini kiwanda kimoja au zaidi kwa kila siku.

Kwa ujumla, Mkurugenzi Teri amewahimiza Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji, akieleza kuwa mazingira ya uwekezaji yameboreshwa kwa kiasi kikubwa. Pia, amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake katika maboresho ya sheria kama Sheria ya Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje na Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 2022, ambazo zimeleta vivutio vya kikodi kwa wawekezaji.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda, amesema kuwa safari ya kikazi iliyowaleta wafanyabiashara 60 kutoka Japan nchini Tanzania inalenga kuvutia uwekezaji mkubwa hasa katika sekta ya miundombinu.

Ameendelea kwa kusema kuwa wawekezaji hao wamebobea katika maeneo mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya kama barabara, madaraja, viwanja vya ndege, miundombinu ya afya na maji, hivyo matarajio ni makubwa katika kupata uwekezaji kutoka kwao.

Pia amebainisha kuwa wawekezaji hao wamesema watawekeza kwenye kongani ya viwanda ilivyopo Bagamoyo mkoani Pwani na kwamba aina ya uwekezaji unaotarajiwa ni wa ubia kati ya wawekezaji hao na Watanzania.

“Licha ya wawekezaji haawa kuwa na mtaji na wataalamu wao wenyewe wa kutekeleza miradi, lakini uwekezaji watakaoufanya hapa ni wa ubia kwa kuungana na Watanzania” alisema Balozi Luvanda

Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mheshimiwa Yasushi Misawa, ameeleza kuwa uhusiano kati ya Japan na Tanzania umedumu kwa miaka mingi, na akaongeza kuwa makampuni mengi kutoka Japan yanaendelea kuja kuwekeza nchini. Alisisitiza kuwa uwekezaji huo utasaidia kukuza uchumi wa Tanzania kupitia sekta mbalimbali, huku ushirikiano wa kibiashara ukiendelea kuimarika zaidi.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka Japan ulikuwa na thamani ya dola milioni 11.2. Pia, kuna kampuni 51 kutoka Japan ambazo tayari zimewekeza nchini Tanzania, jambo linalodhihirisha uhusiano mzuri na matarajio makubwa ya ukuaji wa uwekezaji wa kigeni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!