Latest Posts

TRA IRINGA YAVUKA LENGO LA MAPATO, YAKUSANYA SH. BILIONI 20.11 KWA MIEZI 3

 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa imekusanya Sh. bilioni 20.11 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba 2026, kiasi ambacho ni sawa na ufanisi wa asilimia 138 ya lengo la Sh. bilioni 14.4 lililowekwa kwa kipindi hicho.

Hayo yameelezwa leo, Oktoba 8, 2026, katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yaliyofanyika katika viwanja vya Stendi ya Zamani, Manispaa ya Iringa, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, alikuwa mgeni rasmi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Sitta amewahimiza wafanyabiashara kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati, akisisitiza kuwa mapato yatokanayo na kodi ni muhimu katika kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake na kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Gwamaka Pholld, amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanajisajili na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), kuwasilisha ritani kwa wakati na kutoa risiti kwa wateja kila wanapouza bidhaa au kutoa huduma.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Sindai Michael Kajori, amesema maafisa biashara wa halmashauri hiyo wameendelea kupata ushirikiano mzuri kutoka TRA katika ukusanyaji wa mapato, hali ambayo imechangia kuimarisha mapato na kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Iringa, Peter Felix Utalo, aliiomba TRA kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara ili kuongeza uelewa wao na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali.

Aidha, Utalo ameomba TRA kupitia upya suala la Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT) katika biashara za hoteli, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kuboresha mazingira ya biashara katika sekta hiyo.

Wiki ya Huduma kwa Wateja ni sehemu ya juhudi za TRA za kuwafikia walipakodi, kutoa elimu kuhusu masuala ya kodi na kusikiliza changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa wajibu wao wa kikodi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!